Michezo

Mganda Chesang’ avunja utawala wa Kenya mita 10,000

April 9th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MGANDA Stella Chesang’ amevunja utawala wa Kenya katika mbio za mita 10,000 za Michezo ya Jumuiya ya Madola uliokuwa umedumu tangu mwaka 1998 kwa kunyakua dhahabu nchini Australia, Jumatatu.

Kenya, ambayo ilikuwa imenyakua mataji ya mbio hizi za mizunguko 25 kupitia Esther Wanjiru mwaka 1998, Salina Kosgei (2002), Lucy Kabuu (2006), Grace Momanyi (2010) na Joyce Chepkirui (2014), imeridhika na fedha kupitia Stacy Ndiwa.

Wakenya Ndiwa, Sandrafelis Chebet na Beatrice Mutai walikuwa bega kwa bega katika kundi la kwanza kwa muda mrefu kabla ya Chesang’ kuwacha wapinzani wake hoi alipochomoka katika mzunguko wa mwisho na kubeba taji kwa dakika 31:45.30.

Ndiwa alikamilisha kwa dakika 31:46:36, huku Mganda Mercyline Chelangat akifunga tatu-bora (31:48.41). Mutai (31:49.81) na Chebet (32:11.92) walimaliza katika nafasi za nne na 10, mtawalia.

Kenya sasa ina medali tatu baada ya kupata shaba Jumapili kupitia Edward Zakayo (mita 5,000) na Samuel Gathimba (matembezi ya kilomita 20).