Dondoo

Mganga alazimika kurudisha mbuzi wa mteja

March 31st, 2019 1 min read

 Na MIRRIAM MUTUNGA

NJUKINI, TAITA TAVETA

MGANGA wa hapa alijipata pabaya baada ya jamaa kupiga kambi kwake akimtaka amrudishie mbuzi wake kwa sababu hirizi aliyompa haikufanya kazi.

Jamaa alidai kwamba mganga huyo hakumsaidia kamwekupata mke na lazima arudishe mbuzi aliyempa kama malipo.

Penyenye zinaarifu kuwa juzi jamaa alimwendea ‘daktari’ huyo na kumtaka amtibu hili kupata jiko kwa haraka.

Inasemekana kuwa jamaa alitaka kuasi ukapera baada ya kuishi bila mchumba kwa muda mrefu. Mganga alimwitisha mbuzi mweusi na kumpa hirizi na kumuahidi kwamba angepata mke baada ya miezi mitatu.

Hata hivyo jamaa aliendelea kukaukiwa hata baada ya miezi sita.? Siku ya tukio, jamaa alifika nyumbani kwa mganga huyo akiwa mwingi wa hasira huku akilalamika kuwa huduma zake zilikuwa feki.

Jamaa alimuangalia mganga kwa macho makavu na dharau tokea utosini hadi kwenye miguu na kuanza kumfokea akimtaka amrudishie mbuzi wake.

“Kazi yako ni kupora watu tu, tangu nilipotoka hapa kwako sijaona mabadiliko hata kidogo. Sasa nataka unirudishie mbuzi niliyekuletea mara moja,”jamaa alisema.

Mganga kuona hayo alianza kumzima jamaa na kumwambia arudi nyumbani kisha asubiri wiki moja na mambo yatakuwa sawa. Hata hivyo jamaa alikataa maneno hayo na kumwambia mganga kuwa hatabadilisha msimamo wake.

“Mzee, usinipotezee wakati, mimi nimesema na siongei tena, nipe mali yangu na ubaki na dawa yako, siitaki tena,” jamaa aliendelea kusema kwa hasira.

Mganga hakuwa na la kufanya ila kumrudishia jamaa mbuzi wake. Jombi aliondoka huku akimrushia maneno mganga huyo na kusema kuwa hatawahi kutia guu lake kwa mganga tena.