Habari Mseto

Mganga aliyefumaniwa akiwa uchi kukaa rumande zaidi

September 15th, 2020 1 min read

Na Lucy Mkanyika

MGANGA wa dawa za kienyeji mwenye umri wa miaka 71 katika Kaunti ya Taita Taveta, jana alishtakiwa katika mahakama ya Wundanyi kwa kupatikana akitembea akiwa uchi kwenye boma la mtu mmoja.

Duncan Masaka ambaye anayo leseni ya kuendesha tiba kwa kutumia dawa za mitishamba, alitenda kosa hilo katika kijiji cha Ronge eneo la Kishau majuma mawili yaliyopita.

Siku ya tukio, iliwalazimu polisi waingilie kati na kumwokoa baada ya umati kumvamia ukimlaumu kwa kuendeleza urogi nyumbani kwa mtu huyo. Bw Masaka pia ni mganga ambaye anaaminika kuwa na uwezo wa kuleta mvua hasa nyakati za ukame.

Hapo jana, akiwa mbele ya hakimu mkazi Emmily Nyakundi, alikubali mashtaka hayo ya kuvuruga amani ya watu na sasa atazuiliwa kwa miezi miwili kama njia ya kumhakikishia usalama wake, kwani raia bado wanadaiwa kumwinda.

Ripoti iliyowasilishwa mbele ya Bi Nyakundi ilibainisha kuwa mzee huyo amekuwa akiwaletea wenyeji mvua na kutoa tiba kwa kutumia miti-shamba tangu 1987.

Pia ilidaiwa amekuwa akifanya kazi na serikali ya kaunti ambapo yeye hushauriwa mara kwa mara kuhusu masuala ya kitamaduni.

Hata hivyo, kwenye ripoti hiyo Bw Masaka alifichua kwamba alikuwa amebugia pombe. Pia alidai ni wakazi ndio walimvua nguo kisha wakamshutumu kwa kushiriki urogi.