Kimataifa

Mganga anaswa kwa kuzika watu wakiwa hai Tanzania

Na MASHIRIKA August 29th, 2024 1 min read

DODOMA, TANZANIA

POLISI nchini Tanzania wanawazuilia watu wanne akiwemo mganga wa kienyeji, kwa tuhuhuma za mauaji ya watu 10 ambao miili yao ilipatikana imezikwa katika maeneo ya mji wa Chemba, Dodoma na mkoa wa Singida.

Baadhi yao waliuawa kwa kunyongwa, kuzikwa wakiwa hai au kuchomwa moto.

Msemaji wa Polisi Tanzania, David Misime, alisema miili tisa kati ya 10 ilizikwa ikiwa imeketishwa kwenye shimo, kitendo kinachoashiria imani ya ushirikina.

Ilibainika kuwa miili mitatu ilizikwa nyumbani kwa mganga huyo katika mkoa wa Singida, ikiwemo ya watoto wawili, wenye umri wa miezi miwili na minne iliyozikwa kwenye zizi la mifugo kati ya Machi na Juni mwaka jana, 2023.

Mmoja wao alitambuliwa kuwa mtoto wa mganga huyo wa kienyeji.

Misime alisema, mganga huyo, Bw Nkamba Kasubi, alishirikiana na polisi kwa kutoa taarifa baada ya uchunguzi kuhusu vifo vya watu watatu waliofukuliwa nyumbani kwake.

Kasubi alionyesha polisi hao alipozika miili mingine sita katika Wilaya ya Chemba na mmoja uliotupwa katika mbuga ya Swangaswanga, Dodoma.

Ripoti ya polisi ilisema mganga huyo alielekeza mmoja wa waathiriwa kutolewa kafara ili pesa za kununua shamba zirudi kwa mnunuzi.

“Mnamo Agosti 27, baada ya mtuhumiwa huyo kukamatwa na kukutanishwa na wenzake, ndipo mganga wa kienyeji Kasubi, alikubali kuongoza polisi katika mji wa Porobanguma, Wilaya ya Chemba na kuonyesha mashimo sita aliyofukia watu wengine aliyowaua na kuwazika,” alisema Misime.

Bw Misime alisema uchunguzi wa msururu wa matukio hayo katika Mkoa wa Singida na Dodoma unaendelea kusaka watu wengine waliotekeleza uhalifu huo.