Dondoo

Mganga apokonya polo mke

June 16th, 2019 1 min read

Na JOHN MUSYOKI

EKALAKALA, MASINGA

MGANGA mmoja maarufu eneo hili alikiona kilichomtoa kanga manyoya shingoni alipolimwa na jombi kwa kumteka mke wake.

Duru zinasema mke wa jamaa alitoroka usiku na akaanza kumtafuta lakini hakumpata hadi pale alipoamua kwenda kwa mganga amsaidie kwa kupiga ramli.

Cha kushangaza ni kwamba jamaa alipigwa na mshangao mkubwa alipopata mke wake akimpikia mganga chakula.

Jombi alipandwa na mori na kuanza kumfokea mganga kabla ya kumtwanga.

“Kwa nini ulimeweka mke wangu hapa kwako? Wewe ni mganga sampuli gani. Leo ni leo msema kesho ni mwongo. Nitakuvunjavunja mpaka useme ukweli wa mambo. Mke wangu anafanya nini hapa kwako?” jamaa aliuliza huku akitokwa na jasho shingoni kwa hasira.

Mganga alijaribu kujitetea lakini dua zake ziliambulia patupu.

“Mke wako alinitembelea jana usiku. Giza lilipoingia aliogopa kurudi nyumbani akiwa peke yake nami nikampa chumba cha kulala. Sasa amejitolea kunipikia staftahi kabla ya kuondoka. Tafadhali usinidhuru hata kidogo,” mganga alisikika akimwambia jamaa.

Jamaa alimrukia mganga na kumtwanga bila huruma akimlaumu kwa kumteka mke wake.

“Leo utashika adabu. Utasema ukweli wa mambo ulikuwa unafanya nini na mke wangu,” jamaa alifoka.

Mke wa jamaa kuona vita vilikuwa vimechacha, alitimua mbio mfano wa mtu aliyefukuzwa na pepo na kuingia mitini.

Jamaa alimwacha mganga na maumivu baada ya kumfunza adabu na kuanza kumsaka mkewe.

Wakazi walishangaa kwamba mganga alikuwa amemweka kinyumba mke wa mwenyewe na wakaapa kumfukuza katika kijiji chao.

Haikujulikana iwapo jamaa alifanikiwa kumpata mke wake au ikiwa wakazi walimfukuza mganga huyo.