Dondoo

Mganga asakwa kwa dai la ‘kufunga’ mvua

August 7th, 2018 1 min read

Na DENNIS SINYO

Mlima Elgon, Bungoma

MGANGA mmoja aliyekuwa akihudumu eneo hili alilazimika kujificha kwenye mapango baada ya wanakijiji kumvamia wakidai alikuwa amezuia mvua kunyesha.

Inasemekana mganga huyo kutoka taifa jirani alikuwa akidai kwamba alikuwa na uwezo wa kufanya mvua kunyesha au kuzuia isinyeshe.

Penyenye zasema kwamba jamaa huyo alikuwa amehudumia mkazi mmoja aliyekataa kumlipa Sh5,000 kisha akatisha kufanya jambo ambalo wanakijiji wote wangejutia maishani mwao.

“Kama sitapata pesa zangu kwa muda wa siku saba, mjue kila mtu hapa atajuta. Sitaki kujua utatoa wapi pesa ila mimi ninataka kulipwa kabla ya juma kumalizika,’’ alitishia mganga huyo.

Inasemekana kiangazi kilianza kushuhudiwa eneo hili huku wakazi wakishangaa shida ilikuwa nini. Wanakijiji walianza kutamauka mimea yao ilipoanza kunyauka na kuharibika.

Hapo ndipo iliposhukiwa ni mganga aliyekuwa chanzo cha masaibu hayo hasa kufuatia vitisho vyake baada ya kutolipwa deni.

Kulingana na mdokezi, wanakijiji waliandamana hadi kwa mganga huyo wakiimba nyimbo za kumkejeli na kutishia kumpa funzo la mwaka.

Baada ya kupata fununu kwamba maisha yake yalikuwa hatarini, jamaa huyo alichomoka kupitia dirisha la nyuma na kutimua mbio kuelekea mapango yaliyo milimani. Wanakijiji walipofika kwake, hawakumpata kwani alikuwa

tayari ametorokea usalama wake na kujificha kwenye mapango.

Wakazi hao waliapa kutumia njia zote kumsaka na kumcharaza mganga huyo kwa kuwaletea mateso.

“Hatutalia wakati mtu anakuja hapa na kutuletea shida. Atakiona cha mtema kuni. Nimepoteza kila kitu shambani kutokana na ukosefu wa mvua. Hasara niliyopata ni zaidi ya Sh300,000,’’ alisema mkulima mmoja.