Dondoo

Mganga ataka nguo za marehemu

December 28th, 2019 1 min read

Na JOHN MUSYOKI

KYETENI, MASINGA

KIOJA kilishuhudiwa baada ya mazishi hapa mganga alipotimuliwa mbio alipotaka akabidhiwe nguo za marehemu.

Inasemekana baada ya mazishi mganga huyo alibaki nyumbani na kuelezea watu wa boma kwamba alitaka mavazi ambayo marehemu alikuwa akivaa alipokuwa hai.

Watu wa familia kusikia hivyo, walipigwa na mshangao mkubwa na kuanza kumkabili mganga huyo licha ya kutoa vitisho.

“Wewe ni nani na unataka mavazi ya marehemu! Hatukujui na marehemu hakuwa na uhusiano na wewe. Toka na uende kabisa,” mzee mmoja alimwambia mganga.

Mganga alianza kutoa vitisho vyake lakini hakufua dafu.

“Mtu asijaribu kunifukuza. Marehemu alikuwa mteja wangu wa karibu na tulikuwa marafiki. Tuliahidiana kwamba nitakuwa ninavaa mavazi yake. Mkikataa mtajilaumu wenyewe. Kila nguo ya marehemu ina hirizi niliyompa na haifai kuvaliwa na mtu mwingine isipokuwa mimi tulivyokubaliana naye,” mganga alifoka.

Inasemekana kila mtu katika boma hilo alichukua kila aina ya silaha; si mawe, si panga, si rungu, si nyahunyo na hata kuni kumtwanga jamaa huyo.Baadhi yao walisikika wakilia kwamba huenda jamaa huyo alisababisha kifo cha mpendwa wao ili achukue mavazi yake.

Mganga alipoona maisha yake yalikuwa hatarini na hakuna mtu aliyekuwa na huruma na yeye, alitoka shoti na kupotea..

Watu walibaki kunong’onezana kuhusu kisa hicho huku watu wa boma wakiapa kumchukulia mganga huyo hatua. Mjane wa marehemu alisema hakufahamu mumewe alikuwa akimtembelea mganga kwa miaka zaidi ya 25 waliyokuwa kwenye ndoa.

Hata hivyo haikujulikana iwapo familia ya marehemu ilimwandama mganga huyo.