Mganga ataka shirika limrejeshee Sh18.5m

Mganga ataka shirika limrejeshee Sh18.5m

Na BRIAN OCHARO

MGANGA wa kienyeji, Bw Stephen Vicker Mangira amewasilisha ombi mahakamani kutaka shirika la serikali la kuzuia mali za ulaghai (ARA), liagizwe kumrudishia mamilioni ya pesa na mali zake zilizozuiliwa kwa madai zilipatikana kwa njia za uhalifu.

Hii ni baada ya mahakama kumpata bila hatia katika tuhuma za utapeli wa pesa na ulanguzi wa dawa za kulevya.

Bw Mangira sasa anataka korti iamuru arudishewe Sh18.5 milioni na magari kadhaa ambayo yalizuiliwa na ARA.

Kupitia kwa wakili Kinyua Kamundi, anasema kwamba kwa kuwa ameachiliwa, anapaswa kuregeshewa mali zake, na kuongezea kuwa ARA haikutafuta amri yoyote ya kushikilia vitu hivyo baada ya kuachiliwa huru.

Wakili huyo amekosoa ARA kwa kuendelea kushikilia vitu hivyo akisema huo ni ukiukaji wa sheria unaotoa dhana ya kuwa ana hatia.

“Korti ilisema hana hatia na ikamuachilia huru na uamuzi huo haukuacha nafasi yoyote ya kushikilia mali ya mtu asiye na hatia,” akasema Bw Kamundi.

Bw Mangira aliweka ombi hilo mwezi mmoja baada ya kuachiliwa huru kwa mashtaka 12 ya ulanguzi wa dawa za kulevya, utakasaji wa pesa haramu, na kushukiwa kupata mali kinyume cha sheria.

Alishtakiwa pamoja na washukiwa wengine watatu.

Bw Mangira alitoa ushahidi katika kesi hiyo ya jinai kwamba yeye ni mtaalam wa dawa asili na alipata mali zake kupitia kazi hiyo.

Ili kuendeleza biashara yake, alisema anapata dawa zake kutoka kwa misitu na milima na pia kwa kuelekezwa na ‘malaika’.

Kulingana na rekodi ya korti, mtaalam huyo ana wateja nchini Kenya na ulimwenguni kote, ambao wamethamini kazi yake kwa kumpa pesa taslimu au magari ya kifahari kulipia gharama za matibabu.

Siku ya kukamatwa, Bw Mangira alimwambia Hakimu Mkuu wa Shanzu Florence Macharia kuwa alikuwa na mtoto wake wa miaka 10 wakati alipovamiwa na maafisa wa polisi waliojumuisha wale kutoka Huduma za Kitaifa za Ujasusi (NIS).

Siku hiyo, alipaswa kukutana na marafiki wengine kwenye Hoteli ya Reef, na kwa kuwa mtoto wake alipenda kuogelea, alilipia chumba katika hoteli hiyo.

Alikuwa na Sh20 milioni na kati ya hizo, Sh600, 000 ilipaswa kulipwa kama ada ya shule kwa mtoto wake.

“Fedha zilikuwa kwenye mifuko miwili kwenye buti ya gari langu,” alisema.

Alikana kuwafahamu washtakiwa mwenzake Bw Nabil Loo Mohamed, Bakari kali Bakari na Lilian Martin kabla ya kukamatwa na kushtakiwa kortini mnamo 2017.

Kulingana na ushuhuda wake mbele ya hakimu huyo, polisi walichukua Sh20 milioni iliyokuwa ndani ya mifuko hizo miwili, lakini waliwasilisha tu Sh18.5 milioni kortini.

Alikana kushiriki katika vitendo vyovyote vya uhalifu na kuelezea kuwa alipata utajiri wake kutoka kwa wateja wake ambao walimpa pesa na magari baada ya kuridhika na huduma zake.

Bw Mangira alikanusha kupatikana au kufanya biashara ya dawa za kulevya, kufadhili ugaidi au utapeli wa pesa na kwamba utajiri wake haukuwa unatokana na uhalifu.

Upande wa mashtaka uliita mashahidi 19 kwa jaribio la kuthibitisha makosa 12 ambayo Bw Mangira na washtakiwa wenzake watatu walikuwa wanakabiliwa nayo.

Serikali ilidai Bw Mangira alipata utajiri wake kupitia uhalifu kwa kuhusika katika ulanguzi wa dawa za kulevya.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa wanne hao walikamatwa baada ya ripoti ya ujasusi kuwahusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya huko Nyali.

Hata hivyo, Bi Macharia alisema kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha mashtaka 12 waliyoweka dhidi ya washukiwa hao.

Kwa kosa la utapeli wa pesa, korti ilibaini kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kudhibitisha kuwa washukiwa walifanya uhalifu na kufaidika moja kwa moja au kwa njia nyingine na uhalifu huo.

You can share this post!

Waziri atangaza Sikukuu Jumanne Waislamu wakiadhimisha...

Covid: Uhaba wa vitanda, oksijeni waua wengi Afrika