Dondoo

Mganga atibua njama ya stima yake kukatwa

February 8th, 2019 1 min read

 Na DENNIS SINYO

Majengo, Sabatia

AJENTI wa nyumba za makazi mtaani hapa aliyeenda kukata stima katika nyumba ya mganga, aliondoka ghafla baada ya kufanyiwa mazingaombwe.

Jamaa aliona giza alipokutana na mganga huyo na ikabidi aondoke.? Inasemekana jamaa huyo alifika kwa piki piki kwenye jumba alilokuwa akiishi mganga huyo ili kukata stima. Inadaiwa mganga hakuwa akilipa bili ya stima kwa muda mrefu jambo?ambalo lilisababisha mhudumu huyo kufika kuikata.

Hata hivyo, juhudi zake hazikufua dafu alipoarifiwa kwamba?alikuwa akicheza na moto. Mara tu alipofika kwenye lango la jumba hilo, mkazi mmoja alimtaka aondoke kwani alikuwa akijitia mashakani.

“Usicheze na huyo mtu.Kama huna habari ujue kwamba huyu mtu ni mganga hatari sana kutoka nchi jirani. Kila mtu hapa anamuogopa kwani akiamua kukufanyia kisanga, utajuta maishani mwako,” jamaa aliambiwa.

Hata baada ya kupewa maelezo hayo, mhudumu huyo hakusikia la mwadhini wala la mteka maji msikitini. Aliyatia masikio yake nta Na kuingia ndani ya jengo. Hapo alikutana ana kwa ana na mganga mwenyewe akijiandaa kuwahudumia wateja wake.

Punde tu baada ya kueleza alikuwa amefika kukata stima, jamaa huyo alipewa onyo kali. Alishauriwa?kuondoka mara moja la sivyo ajute maishani.

“Kama unataka?amani, tafadhali nakupa dakika mbili uondoke la sivyo hutaamini kitakachotokea,’’alionya mganga huyo.? Jamaa alianza kutoa jasho kila mahali na kuamua kuwasha piki?piki yake kuondoka kwenye jengo hilo kwa kasi.

Inasemekana aliendesha piki piki hiyo bila kutazama nyuma akihofia kisanga ambacho kingempata.

Kulingana na mdokezi, jamaa huyo alisema alikuwa ameanza kuona giza mara tu alipopewa onyo kuondoka kwa mganga. Baadaye mganga alilipa bili yote bila kushurutishwa.