Dondoo

Mganga azirai mkewe alipookoka

February 20th, 2020 1 min read

Na John Musyoki

KAVATI, Kitui

MGANGA wa hapa alianguka na kuzirai baada ya kugundua kwamba mke wake alikuwa ameokoka katika njama ya kuvuruga biashara yake.

Inaarifiwa kuwa mke wa mganga huyo aliokoka muda mfupi baada ya kuzozana na mume wake akisema hangeendelea kuishi maisha ya giza ambayo mumewe alipenda.

Inasemekana wakati mke wa mganga alipokuwa akitoa ushuhuda kanisani, mume wake alipashwa habari kwamba mkewe alikuwa ameokoka na kutangaza kuwa angemuombea ili aache kazi ya uganga.

Mganga huyo aliposikia hivyo, alianguka na kuzimia. Mke wa jamaa alipofika nyumbani alipigwa na mshangao alipopata majirani wakimpa mume wake huduma ya kwanza. Alipowadadisi walidai mume wake alizimia baada ya kufahamishwa kwamba alikuwa ameokoka.

“Mchukue mume wako huyu. Amezimia punde tu ulipoamua kuokoka na kutangaza kusambaratisha biashara yake kupitia maombi,” jirani mmoja alisema.

Inasemekana licha ya demu kufahamishwa kilichokuwa kimejiri, alipuuza tu.

“Kama ni kuokoka kwangu kunakomfanya azimie, shauri yake. Amelala tu na usingizi wake ukiisha ataamka,” aliwajibu majirani.

Alisisitiza kuwa ataomba hadi mumewe aache kazi ya uganga na kukumbatia maisha ya nuru ya wokovu.

“Hata nyinyi ambao ni wateja wake nitawaombea muokoke,” mama alisema. Majirani waliendelea kumpa mganga huyo huduma ya kwanza licha ya kupuuzwa na mkewe. Jamaa aliporudiwa na fahamu alisema kwamba alihofia mkewe alitoboa siri zake kanisani.

Mkewe alimweleza kwamba alichofanya ni kuwataka waumini waungane naye katika maombi ili naye aokoke na kuacha kazi ya uganga. Jamaa alisema alirithi kazi hiyo kutoka kwa babu yake na hangeiacha kamwe.

Haikujulikana kilichojiri baada ya kioja hicho.