Habari Mseto

Mganga mashakani ndumba zake kushindwa kunasa vipusa

June 11th, 2018 1 min read

KORINDA, BUSIA

Na DENNIS  SINYO

MGANGA mmoja mtaani hapa alitoroka  sokoni baada ya wateja wake kumvamia kutaka kumchapa wakidai alikuwa akiwachezea shere.

Jamaa huyo alikuwa sokoni kwenye mishemishe za kutafutia familia posho wakati vijana wawili walipofika na kumfokea. Vijana hao walidai alikuwa amewatapeli Sh10,000 kwa kuwauzia hirizi bandia. Walidai  jamaa huyo aliwashawishi kwamba alikuwa na dawa  za kuwawezesha wajipatie vidosho bila kutoa jasho.

Vijana hao waliamua kumpa jamaa huyo hela zao na kisha akawapa hirizi kuvalia kila mara wanapowaona vidosho hao. Licha ya kuhakikishiwa matokeo mazuri, vijana hao walitamauka ndumba  zilipokosa kufanya kazi.

Kijana wa kwanza alidai alifuata maagizo ya kalameni  lakini nusura ajitie mashakani. Alidai kipusa aliyekuwa akimezea mate alimgeukia na kutaka kumchapa kofi mbele ya watu.

“Wewe ni mkora sana. Unakula pesa zetu eti unatupa dawa kumbe ni uongo,’’ alifoka kijana huyo. Kijana wa pili naye alichemka vikali pia akidai alichezwa shere.

Vijana hao walitaka kumpa jamaa kichapo wakitaka kurudishiwa pesa zao. Hata hivyo alifaulu kupenyeza  kwenye umati na kuhepa ili kuepuka gadhabu za watu. Jamaa huyo alikuwa akitumia ujanja kuwatapeli wakazi.