Habari Mseto

Mganga wa Kangundo ndani kwa wizi wa magari

October 9th, 2018 1 min read

Na GASTONE VALUSI

MGANGA mashuhuri mjini Tala katika eneo la Kangundo, Kaunti ya Machakos, Jumanne alitiwa nguvuni na maafisa wa polisi kwa madai ya kuhusika katika wizi wa magari.

Zaidi ya maafisa 35 walivamia makazi ya Bi Anne Mutheu (pichani kushoto) mwendo wa saa tano usiku mnamo Jumatatu wakiongozwa na mkuu wa kitengo cha Flying Squad, Musa Yego, ambapo walipekua yake nje mjini Tala hadi jana mwendo wa saa sita adhuhuri.

Maafisa hao waliwahoji watu kadhaa wakiwemo wa familia ya mganga huyo na wafanyakazi wake kuhusu magari yaliyoshukiwa ni ya kuibwa kutoka maeneo tofauti nchini na vilevile vipuri vya magari.

Jana asubuhi, wakazi wa eneo hilo walifika katika makazi ya mganga huyo baada ya kudokezewa kuhusu uvamizi huo.

Maafisa hao wa polisi walikuwa wamejihami vikali na walifika katika makazi hayo wakitumia magari saba.

Bi Mutheu alionekana akitembea kutoka kona moja hadi nyingine ya makazi yake akiandamwa na maafisa wa polisi huku akingea kwa simu.

Akiwahutubia wanahabari baada ya operesheni hiyo, Bw Yego alisema walimtia mbaroni Bi Mutheu na mshukiwa mwingine.

“Tumepata injini kadhaa za magari, vipuri na vitambulisho 130 vya kitaifa vya watu tofauti ndani ya makazi hayo. Inashangaza kupata vitambulisho hivyo hapa na tunaendelea kuchunguza vilifika hapa kwa njia gani,” akasema Bw Yego.

Bi Mutheu amekuwa akigonga vichwa vya habari kwa umaarufu wake wa kuwa na utajiri mkubwa.

Watu mashuhuri wakiwemo wanasiasa wamekuwa wakitafuta huduma zake za uganga.