Habari Mseto

Mganga wa TZ anayedai kufufua maiti akamatwa Taveta

July 30th, 2019 1 min read

Na LUCY MKANYIKA

POLISI mjini Taveta, Kaunti ya Taita Taveta wamemtia mbaroni mwanamume aliyedai kumfufua kijana aliyefariki miaka miwili iliyopita.

Maafisa wa polisi walilazimika kuingilia kati baada ya umati mkubwa wa watu kufurika katika kijiji cha Bura Ndogo ili kuona maajabu hayo.

Mkuu wa polisi wa Taveta, Bw Lawrence Marwa, alisema kuwa wanamhoji mwanamume huyo ambaye anadaiwa kuwa mganga kutoka nchi jirani ya Tanzania.

Bw Marwa alisema kuwa kulingana na stakabadhi za uhamiaji za mwanamume huyo, aliingia humu nchini ili kufanya ukulima.

Polisi tayari wameanzisha uchunguzi kuthibitisha ikiwa kijana anayedaiwa kufufuliwa mnamo Jumapili alikuwa amefariki na kuzikwa.

“Chifu na maafisa wa polisi wamezuru kaburi la marehemu na kuthibitisha kuwa halijafukuliwa. Vilevile tumeona kijana ambaye inadaiwa alifufuliwa,” akasema.

Afisa huyo alisema kuwa kulingana na rekodi za polisi, kijana anayedaiwa kuwa alifufuliwa alijinyonga na serikali kutoa kibali cha mazishi.

“Rekodi zinaonyesha kuwa kijana alijinyonga na polisi wakaenda wakathibitisha kisa hicho. Haya ya yeye kuwa amefufuka hatuelewi,” akasema.

Wanakijiji vilevile walisema kuwa marehemu alifariki mnamo 2017 baada ya kujinyonga.

Walioshuhudia kisa hicho walisema kuwa kijana huyo wa miaka 16 alizikwa katika makaburi ya Taveta miaka miwili iliyopita.

“Hatutamwachilia mwanamume huyu hadi pale tutakuwa tumemaliza uchunguzi wetu,” akasema Bw Marwa.

Alisema kuwa familia inayodai kuwa mwana wao alifufuliwa itahojiwa ili kusaidia katika uchunguzi.