Habari za Kitaifa

Mgawanyiko chama cha Ruto, UDA

April 8th, 2024 1 min read

NA JOSEPH OPENDA

DALILI za mapema za mgawanyiko zimejitokeza ndani ya chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) kaunti ya Nakuru, baada ya mbunge wa zamani wa Bahati Kimani Ngunjiri kutangaza kuwa amegura chama hicho kuelekea uchaguzi wake wa mashinani.

Mwanasiasa huyo mkongowe alisema uamuzi wake unatokana na kudorora kwa umaarufu wa chama hicho katika eneo hilio.

Bw Ngunjiri ni ambaye ni mmoja wa wandani wa Rais William Ruto alioteua kuwa Waziri Msaidizi (CAS), alidai tawi la UDA Nakuru limeingiliwa na watu wanaoongozwa na masilahi ya kibinafsi ambao wamevuruga usimamizi wa chama hicho.

“Hali hii imesababisha chama cha UDA kupoteza ushawishi katika kaunti hii ya Nakuru na eneo zima la Kati mwa Bonde la Ufa,” akasema Bw Ngunjiri

Mwanasiasa huyo mbishani alidai kuwa watu hao pia waliwapiga kumbo wanachama wengine wenye maoni tofauti na yao.

Aidha, Bw Ngunjiri alisema kuwa wakazi wa Nakuru wamepoteza imani na chama hicho ambacho alidai kimeharibiwa sifa na madai ya ufisadi, mapendeleo na ukabila.

“Nimedumu katika siasa kwa zaidi ya miaka 30 na nimeona jinsi vyama vya awali vilisambaratika. Niliona jinsi KANU, PNU na Jubilee viliporomoko na ninaweza kukuambia kuwa UDA inachukua mkondo sawa na huo. Nitaendelea kumuunga mkono Rais Ruto nikiwa nje ya UDA,” Bw Ngunjiri akasema kwenye mahojiano na wanahabari.