Siasa

Mgogoro wa Sudi ulivyofichua siri ya vita vya UhuRuto

September 20th, 2020 3 min read

Na LEONARD ONYANGO

KIZAAZAA wakati wa kukamatwa kwa Mbunge wa Kapseret, Bw Oscar Sudi kimefichua namna uhusiano baina ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto ulivyodorora kwa kiasi kikubwa.

Maafisa wa Polisi wiki iliyopita walishindwa kumkamata Bw Sudi kutokana na madai kwamba walizuiliwa na maafisa wa usalama wanaolinda Naibu wa Rais.Kwa mujibu wa ripoti, maafisa hao ndio walimtorosha Bw Sudi ili kumnusuru kutoka mikononi mwa polisi.

Maafisa hao, hata hivyo, waliachiliwa huru huku polisi wakiendelea kufanya uchunguzi ili kubaini kwa nini maafisa hao wanaolinda watu mashuhuri walikuwa nyumbani kwa Bw Sudi.

Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa alinukuliwa akisema kuwa maafisa hao walikuwa wamealikwa na Bw Sudi kwa ajili ya chakula cha jioni.

Maafisa hao walikuwa wamesindikiza Naibu wa Rais hadi nyumbani kwake katika eneo la Sugoi, Kaunti ya Uasi Gishu, kabla ya kuelekea nyumbani kwa Bw Sudi.

Chama cha ODM kikiongozwa na kinara wake Raila Odinga kimemtaka Naibu wa Rais kuwajibika na kuwaeleza Wakenya kwa nini maafisa wake walijipata nyumbani kwa mbunge wa Kapseret.

Wadadisi wa masuala ya siasa wanasema kuwa kizaazaa hicho ni ithibati kwamba Dkt Ruto amepoteza usemi ndani ya Jubilee.“Bw Sudi ni mtetezi mkuu wa Dkt Ruto na kuna uwezekano kwamba alijaribu kumwokoa mbunge huyo bila mafanikio.

“Hilo linaashiria namna naibu wa rais amepoteza ushawishi serikalini na hata hawezi kutoa amri kwa afisa yeyote wa serikali,” anasema BwGeorge Mboya , mdadisi wa siasa.

Kudorora kwa uhusiano huo kumesababisha Naibu wa Rais Ruto kuanza ‘kujitenga’ na serikali ya Uhuru Kenyatta ili kujiongezea umaarufu wa kisiasa.

Dkt Ruto amekuwa akitoa kauli zinazofanya serikali ya Rais Kenyatta kuonekana kama isiyojali masilahi ya wananchi maskini, iliyojaa ufisadi na dhuluma.Dkt Ruto, hata hivyo, atakuwa ajihusisha na miradi mizuri inayoanzishwa na serikali ya Jubilee.

Hilo lilibainika wiki iliyopita ambapo Baraza la Mawaziri liliidhinisha kubuniwa kwa hazina ya kutoa mikopo kwa wafanyabiashara wadogo walioathiriwa na janga la virusi vya corona.

Kulingana na Baraza la Mawaziri, Sh10 bilioni zitatolewa kama mikopo kwa wafanyabiashara wadogo kat yam waka huu wa fedha wa 2020/2021 na mwaka wa 2021/2022.

Baada ya kikao hicho, wanasiasa wa Tangatanga walimmiminia sifa tele Dkt Ruto wakisema kuwa uwepo wake katika Baraza la Mawaziri ndio ulisababisha serikali kuidhinisha fedha hizo zinazolenga wananchi wa mapato ya chini.

Naibu wa Rais pia anaonekana kuanza kumshambulia Rais Kenyatta moja kwa moja tofauti na hapo awali ambapo alizungumza kwa mafumbo na kuelekeza hasira zake kwa Bw Odinga.

Alipokuwa akizungumza Jumapili iliyopita mjini Kitengela, Kaunti ya Kajiado, Dkt Ruto alisema kuwa hatishiki yuko tayari kukabiliana na ‘system’- yaani watu wenye ushawishi mkubwa serkalini.

“Kuna watu wanatutisha ati wako na ‘system’, na mimi niliwaambia tuko na Mungu na tuko na wananchi. Wakuje na system na sisi tuko tayari tunawangojea,” Dkt Ruto akaambia wafuasi wake.

Naibu wa Rais pia amejitokeza na kupinga Rais Kenyatta huku akisema kuwa Mpango wa Maridhiano (BBI) unalenga kugawanya Wakenya na ni mradi wa watu kunufaisha wanasiasa wachache.

“Wakennya wanataka ajira, huduma bora za matibabu na viongozi ambao watawawezesha kujiinua kimaendeleo sio kugawanywa kwa masilahi ya watu binafsi,” akasema Dkt Ruto.

Rais Kenyatta, amekuwa akikwepa kumjibu Dkt Ruto huku akishikilia kuwa huu si wakati wa siasa.Akizungumza Alhamisi alipokuwa akizindua mradi wa Sh1.9 bilioni wa kutengeneza madawati, Rais Kenyatta alisema kuwa hana wakati wa kujihusisha bali anashughulikia maendeleo.

Naibu wa Rais amekuwa akikutana na viongozi wa madhehebu mbalimbali ili kujipatia uungwaji mkono.Ijumaa, Dkt Ruto alikutana na viongozi wa Kanisa la African Church of the Holy Spirit la Embu waliokuwa wameandamana na mbunge Maalumu Cecily Mbarire.

Baadaye alikutana na aliyekuwa mbunge wa Starehe Margaret Wanjiru ambaye pia ni kiongozi wa kanisa la Jesus Is Alive Ministries.

Wadadisi wanasema kuwa Dkt Ruto anataka kuvutia viongozi wa makanisa upande wake sawa na alivyofanya 2010 wakati wa kupinga rasimu ya katiba mpya.

Viongozi wa makanisa walikataa rasmu ya katiba wakidai kuwa ilikuwa ikiendeleza ushoga. Naye, Dkt Ruto aliipinga kutokana na kigezo kuwa ingetoa mwanya kwa watu kupokonywa mashamba yao.