Habari Mseto

Mgomo wa JKIA ulivyozimwa

February 7th, 2019 2 min read

CHARLES WASONGA Na BERNARDINE MUTANU

Abiria wa ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (Nairobi) walipata afueni baada ya wahudumu kuondoa mpango wa kugoma.

Mgomo huo ulitarajiwa kuanza Jumatano na ulikuwa umeitishwa kulalamikia kutwaliwa kwa usimamizi wa JKIA na Shirika la Ndege la Kenya Airways.

Mgomo huo ulisitishwa Jumanne jioni baada ya wafanyikazi hao kukutana na Waziri wa Uchukuzi na Miundo Msingi James Macharia.

Bw Macharia aliwahakikishia kuwa hawatapoteza kazi kutokana na hatua hiyo. Baadhi ya wahudumu waliotarajiwa kujiunga na mgomo huo ni wahudumu wa ndege na wale uhudumu katika maduka yaliyomo ndani ya uwanja huo.

“Ningependa kumshukuru waziri wa uchukuzi kwa kutuhakikishia kuwa hatutafutwa kazi baada ya JKIA kutwaliwa na KQ. Tumekubali kutogoma kutoa nafasi kwa washikadau wote kujadiliana,” alisema katibu Mkuu wa chama cha wafanyikazi wa viwanja vya ndege(KAWU) Moss Ndiema.

Wafanyakazi walihofia kuwa huenda mpango huo ungepelekea baadhi yao kufutwa kazi au kupunguziwa mishahara.

Akitangaza kusimamishwa kwa mgomo huo Jumanne jioni Katibu Mkuu wa KAWU Moss Ndiema alisema kwamba wizara ya uchukuzi imewahakikishia  kuwa wafanyakazi hawatapoteza kazi zao ikiwa mpango huo utakamilishwa.

“Tumekubali kusimamisha mgomo kwa muda, bali sio kuufutilia mbali, baada ya kupata hakikisho kutoka kwa Waziri wa Uchukuzi James Macharia kwamba kazi za wanachama wetu zitasalia salama hata baada ya KQ kuchukua usimamizi wa uwanja wa JKIA,” Bw Ndiema akawaambia wanahabari katika makao makuu ya wizara hiyo, Nairobi.

Wafanyakazi ambao walikuwa wamepanga kugoma, kuanzia jana, ni wale wa kitengo cha mizigo, wahudumu ndani ya ndege, waelekezi wa abiria na wanaohudumu katika maduka ya “duty-free”.

Bw Ndiema alifafanua kuwa mgomo wao umesimamishwa kwa muda siku 60 pekee, akisema wanataraji kuwa baada ya muda huo, KQ na KAA zitakuwa zimekubaliana kuhusu muundo wa ushirikiano huo.

Wiki jana chama cha KAWU kilitoa ilani ya siku saba ya kufanya mgomo kuilazimisha usimamizi wa shirika hilo la ndege kufutilia mbali mpango huo kwa hufo ungepelea wanachama wao 20,000 kupoteza ajira.

Lakini jana, Waziri Macharia alisema Serikali inaunga mkono mpango huo wa KQ kutwaa usimamizi wa uwanja wa JKIA, akisema utapelekea kuimarisha faida za shirika hilo.

“Ningependa kutoa uhakikisho kwamba mpango huo utaimarisha hudumu na faida katika JKAI na kwamba wanafanyakazi hawatapoteza kazi zao. Hata hivyo, majadiliano kuhusu utekelezaji wa mpango huu bado yanaendelea,” Bw Macharia akasema.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU) Francis Atwoli na Katibu wa wizara Bi Esther Koimett.