Habari Mseto

Mgomo wa madereva wa masafa marefu wanukia

June 17th, 2020 1 min read

Na MISHI GONGO

CHAMA cha madereva wa masafa marefu humu nchini kimetangaza kuanza rasmi mgomo wao wa kitaifa kufikia leo saa sita usiku- kuingia Alhamisi – kuishinikiza serikali kutekeleza matakwa yao.

Mwenyekiti wa chama hicho Roman Waema amewataka madereva wote popote watakapokuwa kufikia muda huo, kuweka kando magari yao na kusubiri hadi pale ambapo serikali itakuwa tayari kuwasikiliza.

Akizungumza na wanahabari nje ya kituo cha ukaguzi wa magari cha Miritini kinachotumika kama kituo cha upimaji wa madereva hao virusi vya corona, Waema amedai kuendelea kunyanyaswa kwa madereva wa humu nchini kutokana na kuendeshwa kwa mwendo wa kobe mchakato wa kuwapima madereva hao.

Amedai hiyo ni njama ya serikali kuondoa madereva barabarani na uchukuzi wa mizigo kuendeshwa kwa njia ya SGR kwani kutokana na agizo la kila dereva kupimwa kabla ya kuondoka katika bandari ya Mombasa.

Amesema hali hii inawafanya wengi kutoendelea na kazi hiyo kwa kukosa vyeti kuonyesha hawana virusi hivyo.

Wameishinikiza serikali kuongeza vituo vya upimaji wa madereva katika maeneo mbalimbali ya taifa akitolea mfano kituo hicho cha Miritni ambapo ni madereva 100 pekee waliopimwa tangu Jumatatu kinyume na matarajio ya maderva 400 kwa siku.

Kwa upande wake afisa mkuu mtendaji wa chama cha wasafirishaji wa mizigo humu nchini KTA Dennis Ombok ameunga mkono malalamishi ya madereva hao, akisema kama wamiliki wa magari wameamua kuegesha magari hayo hadi pale malalamishi ya madereva hao yatakaposikilizwa.

Ombok amesema licha ya madereva hao kuwa viungo muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa taifa, wanaendelea kupuuzwa.