Habari za Kitaifa

Mgomo wa walimu wa JSS wazaa matunda Bunge likisema waajiriwe

May 28th, 2024 2 min read

Na EDWIN MUTAI

JUMLA ya walimu wanagenzi 26,000 ambao wamekuwa wakihudumu kupitia ajira ya kandarasi tangu mwaka jana sasa hawatalazimika kusubiri hadi Januari 2025 ili kupewa kazi ya kudumu.

Hapo Jumatatu, Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Elimu na Utafiti iliafikia kuwa walimu hao wa Sekondari ya Msingi (JSS) ambao wamekuwa wakishiriki mgomo, sasa wataajiriwa kuanzia Julai 1, 2024.

Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Tinderet, Julius Melly, ilifuta mpango wa awali wa Tume ya Huduma kwa Walimu Nchini (TSC) wa kuwapa walimu hao kazi mwakani. Walimu hao wa JSS wamekuwa wakigoma tangu muhula huu uanze ili kushinikiza TSC iwape ajira ya kudumu.

Bw Melly aliiambia kamati ya bajeti kuwa Sh8.3 bilioni zimetengwa kuwapa walimu hao ajira ya kudumu.

“Kuanzia mwaka ujao wa kifedha, TSC inafaa kujiandaa kukamilisha mpango huo wa uajiri kwa sababu pesa sasa zimetengewa shughuli hiyo,” akasema Bw Melly akitoa wasilisho lake mbele ya kamati ya bajeti kuhusu hela ambazo wizara ya elimu imetengewa katika bajeti ya 2024/25.

“TSC itawapa walimu 26,000 wa JSS ajira ya kudumu kuanzia Julai 2024 na si Januari 2025 jinsi ilivyokuwa imependekezwa,” akasema.

Mgomo wa walimu wa JSS umeathiri shughuli za masomo katika shule mbalimbali tangu muhula huu uanze. Wiki jana, TSC iliwaandikia walimu hao 7,357 barua ikitaka wajitetee kuhusu hatua yao ya kutofika shuleni.

TSC imekuwa ikiwaajiri walimu kupitia mpango tata wa mkataba tangu 2019 kisha kuwatuma katika shule za msingi na upili.

Wale ambao wapo katika shule za msingi wamekuwa wakilipwa Sh15,000 huku wale wa shule za upili wakipokea Sh20,000 kwa mwezi.

Iwapo wataajiriwa, walimu wa JSS wataanza kupokea Sh36,621 pamoja na marupurupu ya nyumba ya kati ya Sh9,600 na Sh16,000 kutegemea eneo ambako wanafanyia kazi.

Pia wataruhusiwa kuenda mapumziko na kunufaika na mpango wa bima ya afya kwa walimu.

Kamati hiyo ya elimu pia iliitaka TSC itathmini upya idadi ya walimu wanaohitajika kote nchi ili watumie takwimu hizo kutoa mwongozo wa pesa ambazo zinahitaji kuwaajiri na kuwatuma shule ambako watafundishia.

Bw Melly aliongeza kuwa Sh4.68 bilioni zaidi zinahitajika kuwaajiri walimu 20,000 zaidi wa JSS mwaka wa fedha unaoanza mnamo Julai 2024.

Mbunge huyo wa Tinderet alisema TSC inahitaji Sh1 bilioni kuwapandisha walimu vyeo na Sh13 bilioni zitakazoelekezwa katika nyongeza ya mshahara wao kulingana na mkataba wa maelewano 2021-2025.