Habari

Mgomo wa walimu wazimwa

January 3rd, 2019 3 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MGOMO wa walimu uliotisha kusambaratisha ufunguzi wa shule zaidi ya 20,000 kote nchini ulifutiliwa mbali Jumatano na mahakama ya kuamua mizozo ya wafanyakazi na waajiri (ELRC).

Katika uamuzi wa kihistoria Jaji Byram Ongaya alisema haki za watoto ni jambo linalopasa kushughulikiwa na kila mmoja na kuamuru walimu walimu wafike shuleni asubuhi kuanza mughula wa kwanza 2019.

Agizo la mgomo ulioitishwa Desemba 2018 baada ya kukwama mashauri ya kuangazia masuala tata kuhusu kuhamishwa kwa walimu , kupandishwa vyeo, kujiendeleza kimasomo kwa walimu na kusambaratishwa shughuli za KNUT lilisitishwa.

Lakini Jaji Ongaya aliamuru kinara wa TSC Nancy Macharia na katibu mkuu wa KNUT Wilson Sossion wafike katika afisi ya Leba Alhamisi saa tatu kuendelea na mazugumzo ya kutatua mzozo kuhusu mishahara ya walimu na kuhakimishwa kwa walimu.

Mashauri ya kuboresha maslaha ya walimu yalikwama Oktoba 2018 wakati Bi Macharia alipoomba mashauri yahairishwe kuwezesha mitihani ya kitaifa kuendelea.

Jaji Byram Ongaya. Picha/ Richard Munguti

Jaji Ongaya alisema kutokana na mawasilisho ya mawakili wa Knut , Mabw Paul Muite, John Mbaluto na Hilary  Sigei, ni wazi TSC ndiyo imekwamisha mazugumzo na kupelekea KNUT kuitisha mgomo ambao ungeliathiri elimu ya wanafunzi 12,000,000 kote nchini.

Katika uamuzi ambao uliangazia pande zote Jaji Ongaya aliamuru TSC ifutilie mbali barua za kuwahamisha wanachama wa KNUT waliokuwa wamepelekwa nje ya maeneo wanayowakilisha.

Bw Mbaluto alisema kuwa matawi 10 ya KNUT yalikuwa yameathiriwa.

Jaji huyo alisema mawakili wa KNUT walisema walimu zaidi ya 40 kutoka kaunti ya Nairobi walikuwa wameathiriwa na agizo hilo la TSC.

Jaji Ongaya aliamuru tume ya kuajiri walimu (TSC) isikize  malalamishi ya walimu wakuu 3,094 waliohamishwa Desemba 14, 2018 kabla ya Feburuari 15 2019.

Jaji huyo alisema TSC imekuwa ikifanya mambo kiholela katika usimamizi na kuitaka ifuate muwafaka wa makubaliano kuhusu mishahara na maslahi ya walimu (CBA).

“ Hii mahakama imetilia maanani ushahidi na mawasilisho yote ya KNUT , TSC na Mwanasheria mkuu na kufikia uamuzi kuwa lazima haki za wanafunzi zitiliwe maanani,” alisema Jaji Ongaya.

Mahakama ilikiamuru KNUT isitekeleze vitisho vya kuwataka walimu wagome na “ kwamba wanafunzi wanataka kufika shuleni na kuwapata walimu wawapokee.”

Jaji alisema elimu ya watoto imepewa kipau mbele katika katiba na lazima kila anayejali maslaha ya watoto azingatie kwa ukamilifu haki hiyo.

Mahakama hiyo ya leba ilisema kwamba masuala ambayo walimu wanataka watimiziwe yanaweza kushughulikiwa kupitia majadiliano na ikaagiza pande zote kuendelea na juhudi za upatanishi zinazosimamiwa na kamati iliyoteuliwa na Wizara ya Leba.

Jaribio la walimu, kupitia wakili Paul Muite la kutaka shule kufunguliwa Januari 7, 2019 badala ya Alhamisi lilikataliwa mahakama iliposema ombi lake halikuwa mojawapo ya masuala makuu katika kesi.

Katibu mkuu wa KNUT Wilson Sossion wakati wa kesi. Picha/ Richard Munguti

Bw Muite aliwasilisha ombi baada ya Knut kuagizwa kufutilia mbali mgomo akisema chama kilihitaji muda wa kuwasiliana na wanachama kote nchini.

Hata hivyo, ilikuwa ni ushindi kwa walimu, mahakama ilipositisha uhamisho wa walimu zaidi ya 3094 na kuagiza TSC kuchunguza maombi ya wale waliokuwa tayari wamehamishwa. Mahakama iliagiza kesi hiyo kutajwa Januari 17 ili pande zote kueleza mahakama juhudi za upatanishi zitapokuwa zimefikia.

Mawakili wa TSC Mabw Calvin Ayuor na Timon Oyucho walipinga ombi hilo la kuahirishwa kwa tarehe ya kufunguliwa kutoka  Januari 3 hadi 7, 2019.

“Suala hili halikuwa katika masuala nyeti ambayo KNUT ilikuwa inalalamikia na hivyo shule zitafunguliwa jinsi ilivyokuwa imepangwa Januari 3, 2019,” Jaji Ongaya aliamuru.

Awali, walimu walikuwa wameomba mahakama kufutilia mbali agizo la kuharamisha mgomo ikidai TSC haikuwa na nia ya upatanishi baada ya kususia kikao cha Jumanne.

Mnamo Jumanne, Katibu Mkuu wa chama cha Walimu (Knut) Wilson Sossion alikuwa ameagiza walimu kutofika shuleni zikifunguliwa leo baada ya TSC kususia kikao cha upatanishi.

Alhamisi Bw Sossion alisema Knut itatii agizo la mahakama na akawaagiza walimu kufika kazini kuanza mughula kama ilivyokuwa imeratibiwa.

Knut iliitisha mgomo ikitaka TSC kubatilisha uamuzi wa kuhamisha walimu zaidi ya 3,094 kutoka kaunti wanazotoka na TSC ikaenda mahakamani na kupata agizo kuzuia walimu kugoma.

Lakini Bw Sossion aliagiza walimu kutofika shuleni TSC isipotimiza matakwa yao.

Alisema walimu wangefika mbele ya kamati ya upatanishi iliyoteuliwa na waziri wa Leba Ukur Yattani.

Hata hivyo, mnamo Jumatatu kikao hicho kilitibuka na Knut ikalaumu TSC kwa kutumia mahakama kuhangaisha walimu. Jana, mahakama iliamuru TSC kubatilisha uhamisho wa maafisa wa Knut kutoka matawi kumi waliyochaguliwa kuhudumu. Waziri wa Elimu, Amina Mohammed aliunga TSC na kusema kwamba shule zitafunguliwa leo.

“Tangazo lililotolewa Desemba mwaka jana linadumu. Shule zitafunguliwa kesho (leo) licha ya vitisho vyovyote (vya walimu kugoma) vilivyotolewa,” alisema Bi Mohammed akihutubia wanahabari katika Taasisi ya Ukuzaji wa Mitaala nchini (KICD).

Kutoka kulia: Wakili wa TSC Calvin Ayuor (aliyesimamaa) na mawakili wa KNUT Hilary Sigei , Paul Muite na John Mbaluto (kushoto) wakiwa kortini Jumatano. Picha/ Richard Munguti

Mnamo Desemba, Bi Mohammed alitangaza kuwa shule zitafunguliwa leo badala ya jana (Jumatano) ilivyotangazwa awali.

Awali, Bi Mohammed aliyeandamana na Katibu wa Elimu, Belio Kipsang alisema wizara iliunga msimamo wa TSC kwamba walimu wafike shuleni leo. Hata hivyo, muda mfupi baada ya tangazo lake, Jaji Byram Ongaya aliagiza walimu kusitisha mgomo wao na akaitaka TSC kutowahamisha walimu ambao ni maafisa wa Knut kutoka maeneo waliyochaguliwa.

Kuamuliwa kwa kesi hiyo kulikuwa afueni  kwa walimu kwa vile Jaji Ongaya aliamuru TSC ifuate muwafaka wa CBA uliotiwa saini 2017.

Arifa iliyotumiwa na TSC kuingilia utenda kazi wa walimu ya Mei 2018 ilisitishwa.

Kusitishwa kwa arifa hiyo kumelemaza nguvu za TSC iliyokuwa imejitwika kuchukua hatua bila ya kuishirikisha TSC.

Jaji huyo alisema TSC imekuwa ikihepa majukumu yake kwa kutohudhuria vikao vya masikizano.

Mahakama iliamuru TSC ikome kukwepa majukumu yake kwa vile KNUT imekuwa ikihudhuria vikao vyote katika sehemu ya Naivasha.

Mahakama ilifahamishwa kuwa tangu  Feburari 2018 TSC imekuwa ikiepuka majadiliano hayo yanayoshirikisha wizara ya leba.