Habari

Mgonjwa aliyegundulika kuugua Ebola mjini Goma afariki

July 16th, 2019 1 min read

Na AFP

GOMA, DRC

MGONJWA aliyegundulika kuwa na Ebola katika kisa cha kwanza katika mji wa Mashariki mwa DRC wa Goma amefariki, Gavana wa Mkoa wa Kivu ya Kaskazini amesema Jumanne.

Ni hali ambayo inaibua hali ya wasiwasi katika taifa jirani la Rwanda na pia katika Umoja wa Mataifa.

“Inasikitisha ila ukweli ni kwamba mgonjwa huyo ameaga dunia,” Gavana Carly Nzanzu ameambia waandishi.

Mhanga huyo alitajwa kuwa ni mhubiri aliyekuwa amesafiri kutoka Goma kuenda Butembo – mji ambao umeathirika pakubwa na Ebola.

Huko alihubiri katika makanisa saba na hapo aliwashika watu, wakiwemo wagonjwa, kabla ya kusafiri kwa basi kurejea Goma mnamo Ijumaa wiki jana, kulingana na Wizara ya Afya nchini humo.

Jumapili alienda kwa zahanati akiwa na maumivu na vipimo vikabainisha aliwa na Ebola.

Ni hapo ndipo alitumwa tena Butembo ambako wahudumu wa afya wamejiandaa vilivyo kukabiliana na maradhi hayo.