Habari Mseto

Mgonjwa atuhumiwa kuiba Sh52 milioni

March 14th, 2018 1 min read

RICHARD MUNGUTI

MFANYABIASHARA aliyetolewa katika kitanda cha hospitali alipokuwa amelazwa kupokea tiba alishtakiwa Jumanne kwa kupokea kwa njia ya udaganyifu zaidi ya Sh52.3 milioni na kushindwa kulipa.

Bw Sundip Jagdishroy Patel alifikishwa mbele ya hakimu mkuu katika mahakama ya Milimani Nairobi Bw Francis Andayi na kukanusha mashtaka mawili ya  kupokea pesa kwa njia ya undanganyifu na kupeana hundi akijua akaunti yake haikuwa na fedha za kutosha.

Bw Patel alikana kati ya Desemba 13 , 2013 na Desemba 4, 2014 katika kampuni ya Conex Limited alipokea kwa njia ya udaganyifu Sh52,385, 500 akijifanya alikuwa na uwezo wa kumlipa.

Wakili Nelvil Amolo aliomba mshtakiwa aachiliwe kwa dhamana ya pesa tasilimu isiyo ya kiwango cha juu kwa vile alifikishwa kortini akitolewa hospitali alipokuwa amelazwa.

“Mshtakiwa ni mgonjwa na hawezi kukaa katika rumande ya idara ya magereza. Alitolewa hospitali kujibu mashtaka mawili dhidi yake,” alisema Bw Amolo.

Mahakama ilikabidhiwa stakabadhi za hospitali na kuombwa iwe na huruma na mshtakiwa.

Kiongozi wa mashtaka Solomon Naulikha alithibitisha kwamba “ mshtakiwa alikuwa hospitali na kwamba hawezi kutoroka.”

Alisema Bw Naulikha, “Afisa anayechunguza kesi hii alimtoa mshtakiwa hospitali kujibu shtaka la wizi wa mamilioni haya na kumwandikia mlalamishi Bw Vijay Morjaria  hundi ya Sh52.3milioni akijua hakuwa na pesa za kutosha katika akaunti yake.”

Bw Naulika alisema hundi hiyo ilikuwa inatakiwa kulipwa na Benki ya African Banking Cooperation ABC

Mshtakiwa aliachiliwa kwa dhamana ya Sh200,000 pesa tasilimu awasilishe mdhamini wa Sh500,000.

Kesi itasikizwa mnamo Aprili 4, 2018.

Bw Naulikha aliambia korti mshtakiwa yuko huru kuendea nakala za mashahidi ndipo aandae utetezi wake.