Habari Mseto

Mgonjwa wa mapafu na moyo Baringo aomba msaada anunue oksijeni

June 12th, 2024 2 min read

Na FLORAH KOECH

MGONJWA mmoja katika Hospitali ya Rufaa ya Baringo anaomba msaada wa kununua mtungi wenye oksijeni kumsaidia kupumua baada ya kulazwa kutokana na tatizo la mapafu na moyo tangu Novemba 28 mwaka jana.

Godwin Kemei, 24, ambaye amekuwa akitegemea oksijeni hospitalini, amelemewa na unyonge kufuatia kuwa hospitalini kwa miezi minane sasa. Kijana huyo alipatikana kuwa na ugonjwa wa moyo na pia tatizo kwenye mapafu.

Kinachosikitisha kuwa ni hakuna jamaa wa Bw Kemei kutoka kijiji cha Seretunin ambaye amemtembelea hospitalini kwa muda huo, akionekana ametelekezwa na wanafamilia wake.

Bw Kenei alifiwa na wazazi wake akiwa mdogo sana na aliachwa chini ya uangalizi wa shangazi yake kutoka Keringet Kaunti ya Nakuru pamoja na nduguye mkubwa.

Mauti yalimchukua nduguye mapema mwaka huu wala hakupata nafasi ya kuenda mazishi yake, hali ambayo imemwacha na huzuni tele.

Aidha shangazi yake naye pia aliaga dunia na kumzidishia dhiki mnamo Januari. Wale ambao wamekuwa wakimtembelea ni marafikize na mpenzi wake.

“Bado sijakubali kuwa shangazi yangu aliaga dunia. Sikuhudhuria hata mazishi yake ihali alikuwa mama na babangu tangu utotoni mwangu. Kuwa hospitalini hapa kumenifunza mengi na nawashukuru wahudumu wote kwa kunisaidia,” akasema Bw Kenei ambaye amejaaliwa mtoto mmoja na mpenziwe.

Safari yake ya maradhi yanayomsibu imekuwa ya kuatua moyo tangu 2021. Mwaka huo alienda katika kituo cha afya cha Keringet na ikabainika alikuwa akiugua ugonjwa wa moyo.

Aliufuata mwongozo wa matibabu kila mwezi lakini akalemewa mnamo 2023 huku akitapika pia. Aliendea matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Nakuru ambapo aliambiwa angefanyiwa upasuaji wa kurekebisha mshipa wa njia ya damu kuelekea moyo wake, shughuli ambayo ingegharimu Sh2 milioni.

“Waliniambia kuwa hospitali ya kaunti ingenipa Sh1 milioni kisha kituo cha moyo kigharimie milioni moja nyingine, ningetibiwa. Sikufanikiwa na nikalazimika kurudi nyumbani,” akaongeza.

Mnamo Novemba mwaka jana, alilemewa kupumua na akapelekwa katika kituo cha kimatibabi cha Seretunin, Nakuru kabla ya kuhamishwa hadi Hospitali ya Baringo.

Mnamo Januari 15, 2024 alipelekwa kupokea matibabu Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi ambapo aliacha kitambulisho chake na kufanyiwa vipimo baada ya kulemewa kulipa Sh5,000.

Kilichomshutua ni kuwa vipimo hivyo vilionyesha kuwa hakuwa akiugua ugonjwa wa moyo bali ule wa shinikizo la damu.

“Nilikuwa natibiwa ugonjwa wa moyo tangu 2021 ila vipimo vilionyesha nina shinikizo la damu. Matokeo niliyopewa MTRH na kituo cha moyo Nakuru, yalikuwa tofauti. Niliingiwa na unyonge ila nikalazimika kukubali hali,” akasema.

Hata hivyo, aliendelea na matibabu ya ugonjwa wa moyo kwa sababu alikuwa bado anahisi uchungu.

Bw Kenei hawezi kumaliza dakika 30 bila kutumia oksijeni aliyounganishiwa na iwapo ataruhusiwa kuondoka hospitali bado ataunganishiwa mtungi wenye hewa hiyo.

“Siwezi kununua mtungi wenye oksijeni kwa sababu ni ghali na naomba nisaidiwe,” akasema. Dhiki zaidi ni kuwa mwanawe mwenye umri wa miaka miwili naye hulia zaidi akiongea na babake kwenye simu.

Mhudumu katika Hospitali ya Baringo Martin Ruto alisema Bw Kenei amekuwa mgonjwa wao tangu Novemba mwaka jana, na watamruhusu aondoke hospitalini iwapo ana oksijeni.