Lugha, Fasihi na Elimu

Mhadhara wa kumuenzi Prof Ken Walibora sasa kufanyika Aprili 9

March 29th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

MHADHARA wa Umma wa kumuenzi marehemu Prof Ken Walibora, uliopangiwa kufanyika Aprili 10, 2024, umeratibiwa upya, ambapo sasa utafanyika Aprili 9, 2024.

Kulingana na Prof Ernest Mohochi, ambaye ni miongoni mwa waandalizi wakuu wa mhadhara huo, mabadiliko hayo yanatokana na uwezekano wa sikukuu ya Eid Ul-Fitr kuwa aidha Aprili 10 au Aprili 11.

“Ningependa kuwajulisha kuwa, kutokana na uwezekano wa Sikukuu ya Eid Ul-Fitr kuwa aidha tarehe 10 au 11 Aorili, mhadhara wetu wa kumuenzi Prof Walibora utafanyika tarehe 9 badala ya 10,”  akasema Prof Mohochi, kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Prof Walibora alikuwa msomi, mwanahabari na mwandishi wa vitabu aliyesifika nchini Kenya na duniani kote kutokana na mchango wake mkubwa katika ukuzaji wa lugha ya Kiswahili.

Alifariki kwenye ajali ya barabarani jijini Nairobi mnamo Aprili 2020.

Mhadhara huo umeandaliwa na Kituo cha Taaluma za za Lugha na Utamaduni cha chuo hicho (KITALU), kama kumbukizi kwa msomi huyo, kutokana na mchango mkubwa aliotoa katika “kuwakuza na kuwalea wanafunzi katika masuala ya lugha chuoni humo”.

Mhadhara huo umepangiwa kufanyika kati ya saa nne asubuhi hadi saa saba mchana.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo mwezi uliopita, Naibu Chansela wa chuo kikuu hicho, Prof Odeo Ipara, alisema kuwa tayari kuna kamati inayoendeleza mipango ya maandalizi ya mhadhara huo.

“Ndipo tumeanza mipango ya maandalizi ya mhadhara huo. Tutatoa maelezo kamili kuhusu hali ya matayarisho kuanzia wiki ijayo,” akasema Prof Odeo.

Mtoa mada mkuu atakuwa ni Prof F.E.M Senkoro, aliye Profesa Mstaafu wa Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Wadau mbalimbali wa Kiswahili nchini wamekuwa wakizishinikiza taasisi tofauti kuweka mikakati ya kumkumbuka Prof Walibora, kutokana mchango mkubwa aliotoa katika kuipa utambuzi Kenya duniani kupitia uandishi wa kipekee wa vitabu.