Lugha, Fasihi na Elimu

Mhadhara wa umma kuandaliwa kumuenzi Prof Ken Walibora

March 19th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

WAKEREKETWA wa Kiswahili nchini wanapanga kuandaa mhadhara wa kwanza wa umma kumuenzi marehemu Prof Ken Walibora, aliyefariki Aprili 2020 kwenye ajali ya barabarani jijini Nairobi.

Prof Walibora alikuwa msomi, mwanahabari na mwandishi wa vitabu aliyesifika nchini Kenya na duniani kote kutokana na mchango wake mkubwa katika ukuzaji wa lugha ya Kiswahili.

Mhadhara huo umeratibiwa kufanyika katika Chuo Kikuu cha Kibabii mnamo Aprili 10, 2024, kulingana na taarifa iliyotolewa na Kituo cha Taaluma za Lugha na Utamaduni cha chuo hicho (KITALU).

Mhadhara huo umepangiwa kufanyika kati ya saa nne asubuhi hadi saa saba mchana.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo mnamo Jumanne, Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Kibabii Prof Odeo Isaac Ipara, alisema kuwa tayari kuna kamati inayoendeleza mipango ya maandalizi ya mhadhara huo.

“Ndipo tumeanza mipango ya maandalizi ya mhadhara huo. Tutatoa maelezo kamili kuhusu hali ya matayarisho kuanzia wiki ijayo,” akasema Prof Ipara.

Mtoa mada mkuu atakuwa ni Profesa F.E.M Senkoro, aliye Profesa Mstaafu wa Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Wadau mbalimbali wa Kiswahili nchini wamekuwa wakizishinikiza taasisi tofauti kuweka mikakati ya kumkumbuka Prof Walibora, kutokana mchango mkubwa aliotoa katika kuipa utambuzi Kenya duniani kupitia uandishi wa kipekee wa vitabu.