Habari Mseto

Mhandisi wa programu ashtakiwa kuwadhulumu kimapenzi watoto wake

February 16th, 2024 2 min read

NA RICHARD MUNGUTI

MHANDISI wa programu za kompyuta nchini Marekani ameshtakiwa katika mahakama ya Nairobi kwa kuwadhulumu mabinti wake wawili kimapenzi kati ya 2021 na 2022.

Inadaiwa mshtakiwa aliwatusi wanawe wa kike wa kati ya umri wa miaka miwili na miaka saba katika jimbo la Texas nchini Marekani.

Mahakama ilielezwa baada ya mwanamume huyo kutekeleza uhalifu huo, alirejea humu nchini.

Hakimu mwandamizi Bernard Ochoi aliyesikiliza mashtaka dhidi yake, alifahamishwa mbali na kesi hii ya dhuluma za kimapenzi, mhandisi huyo amekabana koo na mkewe katika Mahakama ya kuamua kesi za watoto katika mahakama hii ya Milimani.

Wakili John Swaka anayemwakilisha mshtakiwa, alifichua kuhusu kesi hiyo nyingine alipoomba mshtakiwa aachiliwe kwa dhamana.

“Kesi hii inayomkabili mteja wangu inatokana na kesi nyingine inayoendelea katika mahakama ya kuamua kesi za watoto,” Bw Swaka alidokeza.

Aliomba mahakama imwachilie kwa dhamana mteja wake kwa sababu alijisalamisha kwa polisi na pia kujileta mahakamani jinsi alivyoagizwa na maafisa wa kulinda usalama.

Mahakama ilifahamishwa mashtakiwa hawezi kutoroka kwa sababu amekuwa akisafiri hadi Marekani na kurudi nchini kwa hiari.

Lakini wakili wa walalamishi wanaotambuliwa kwa herufi MM (mwenye umri wa miaka 7) na IK (mwenye umri wa miaka miwili) Bw Kariuki Karanja, alitofautiana na Bw Swaka.

Wakili huyo alifichua kwamba kesi inayoendelea katika mahakama ya kesi za watoto ni ya mshtakiwa kuomba kuruhusiwa kuwa anawatembelea watoto wake.

“Kesi iliyoko katika mahakama ya kuamua kesi za watoto inahusu mshtakiwa kuomba ruhusa kuwatembelea watoto wake. Haihusu uhalifu huu anaodaiwa kutenda,” Bw Karanja alimweleza hakimu.

Bw Swaka aliomba mshtakiwa aachiliwe kwa dhamana ya Sh20,000 jinsi alivyoachiliwa na polisi.

Ombi hilo lilipingwa vikali na kiongozi wa mashtaka Bw James Gachoka akisema “polisi wanawasilisha hati ya kiapo kueleza sababu za kukataa mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana.”

Hata hivyo Bw Gachoka alisema “polisi wamechelewa kuwasilisha hati ya kiapo ya kupinga ombi la mshtakiwa kuachiliwa kwa dhamana.”

Alikubali mshtakiwa kuachiliwa kwa dhamana ya Sh20,000.

Kesi hiyo itatajwa Februari 20, 2024, kwa maagizo zaidi.