Mhariri asukumwa ndani kwa kudharau mahakama

Mhariri asukumwa ndani kwa kudharau mahakama

NA RICHARD MUNGUTI

MHARIRI wa mtandao wa Tuko, Didacus Malowa jana Jumanne alifungwa jela siku tano kwa kutochapisha habari akiomba msamaha kwa kuripoti kimakosa ushahidi uliotolewa katika kesi ya kashfa ya Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) Aprili 2022.

Hakimu mkuu Eunice Nyuttu anayesikiliza kesi hiyo dhidi ya aliyekuwa katibu mkuu Lilian Omollo na washukiwa wengine alimfunga Malowa bila faini.

Bi Nyuttu alimlaumu mhariri huyo kwa kukataa kuomba msamaha na kufutilia mbali habari hizo za kupotosha katika mtandao huo wa Tuko.

Wakili wa Tuko aliomba mahakama isitishe kumchukulia hatua Malowa akifichua kuna ombi lililowasilishwa katika Mahakama Kuu na wakili Assa Nyakundi akiomba adhabu hiyo iharamishwe.

Bi Nyuttu alielezwa kwamba Mahakama Kuu imeombwa itathmini upya uhalali wa faini ya Sh50,000 aliyotozwa mhariri mkuu wa Tuko ama asukumwe jela miezi sita akishindwa kulipa faini hiyo.

“Kesi hii inahusu kudharauliwa kwa mahakama na kukaidiwa agizo korti iombwe msamaha na kufutiliwa mbali kwa taarifa hiyo ya kupotosha,” wakili huyo alimweleza Bi Nyuttu.

Hakimu alielezwa tayari Malowa ameathirika na amekabiliwa na msongo wa mawazo.

Bi Nyuttu alielezwa suala hilo la kuomba msamaha linafaa kushughulikiwa na wasimamizi wa Tuko na wala sio Malowa ambaye hana mamlaka makubwa kazini.

Na wakati huo huo Bi Nyuttu aliamuru Mhariri Mkuu wa Shirika la Utangazaji nchini (KBC) Millicent Owuor afike kortini leo Oktoba 5, 2022 kuadhibiwa kwa kuchapisha habari za kupotosha kuhusu kesi hiyo ya NYS.

  • Tags

You can share this post!

Bayern Munich waponda Viktoria Plzen nchini Ujerumani na...

Wataalam wakongamana JKUAT kubadilishana mawazo kuhusu...

T L