TAHARIRI: Ipo shida wauguzi kutofahamu lugha

TAHARIRI: Ipo shida wauguzi kutofahamu lugha

Na MHARIRI

UFICHUZI wa Waziri wa Afya Mutahi Kagwe kwamba wauguzi 290 walifeli Kiingereza na kukisa nafasi ya kuajiriwa Uingereza, unaibua maswali kuhusu mfumo wetu wa elimu.

Ni wauguzi 10 pekee katu ya 300 waliopasi mtihani huo wa kuwapima iwapo wanaelewa vyema lugha ya Kiingereza.Na kwa nini wasipumwe? Wauguzi hao walitaka kwenda kufanya kazi Uingereza, ambalo lugha pekee inayotumika kuwasiliana ni Kiingereza.

Ni hatari sana kwa mtu anayetoa huduma za afya kukosa uwezo wa kuwasiliana kwa lugha inayotumiwa na wenyeji.Haijafahamika kama madaktari kutok Cuba walipotaka kuja Kenya walipimwa uelewa wao wa Kiswahili au la.

Kiswahili ni moja kati ya lugha zetu mbili za taifa, zinazotambuliwa na Katiba.Hata kama madaktari hao kutoka Amerika ya Kati walikuwa hawafahamu Kiswahili, baadhi yao walionekana baadaye wakiwasiliana vyema kwa lugha za humu nchini.

Walikuwa wepesi wa kujifunza Kikamba, Kisomali, Kigiryama na kadhalika.Je, wauguzi wetu wana uwezo wa kwenda kujifunza lugha hiyo huko Uingereza? Bila shaka. Hakuna mtu asiyekuwa na uwezo wa kujifunza. Tatizo ni kuwa, mfumo wa Uingereza uko hibyo.

Iwapo unajidai kuwa unaifahamu lugha yao, hawana budi kukupima uwezo wako wa kuiandika, kuisoma na kuizungumza.Mitihani yao mara nyingi huwa ya mambo ambayo hapa Kenya yanafunzwa katika shule za msingi.

Kwa hivyo wauguzi hao kushindwa kukumbuka chochote kuhusu lugha ya Kiingereza, kunatia uoga wagonjwa. Kuna uhakika gani kwamba mambo mazito kuhusu tiba waliyojifunza vyuoni wanayakumbuka, ikiwa hawafahamu nomino, vitenzi na ngeli za lugha?

Uvumbuzi huu sasa uwafunue macho wadau katika sekta ya elimu. Wanaounda mtaala wasizingatie tu mtu kukariri mambo kwa ajili ya mitihani. Kuna Wakenya wengi wanaoonyesha kuwa walupata alama A kwenye mtihani wa Kiswahili, lakini unapowataka waandike angalau aya moja, hawawezi.

Mwanafalsafa Albert Einstein alisema kwamba elimu ni kile kinachosalia akilini baada ya kila kilichofunzwa shuleni kusahaulika. Hapa Kenya, asilimia kubwa ya watu haiwezi kujieleza kwa ufasaha kutumia lugha za Kiingereza na Kiswahili pamoja. Na hili ni tatizo tunalopaswa kulitatua kwa haraka.

You can share this post!

Ananyoa kwa shoka na wateja wamejaa kibao

Nyuki wazua kizaazaa katika kituo cha mabasi cha Machakos

T L