Mhariri wa KBC apata afueni kesi ya kusukumwa jela

Mhariri wa KBC apata afueni kesi ya kusukumwa jela

NA RICHARD MUNGUTI

MHARIRI wa Shirika la Utangazaji Nchini (KBC) amepata afueni ya kutosukumwa jela baada ya Mahakama Kuu kutoa maagizo Ijumaa kesi inayomkabili isitishwe.

Jaji Esther Maina amesitisha kusikilizwa kwa kesi ya kumsukuma gerezani Mhariri wa KBC Bi Millicent Owuor kwa madai alidharau mahakama.

Jaji Maina alisitisha kusikilizwa kwa kesi hiyo dhidi ya Bi Owuor mnamo Oktoba 11, 2022 hadi kesi iliyowasilishwa na wakili Danstan Omari isikilizwe na kuamuliwa.

Katika kesi aliyowasilisha mbele ya Jaji Maina, Bw Omari alisema mhariri huyo hajui makosa aliyofanya licha ya madai ya korti kwamba alikataa kuchapisha msamaha kwa habari za kupotosha kuhusu kesi ya kashfa ya NYS dhidi ya aliyekuwa katibu mkuu Bi Lilian Omollo.

Bw Omari aliomba mahakama isitishe kusikilizwa kwa kesi hiyo hadi pale ushahidi kamili utakapotolewa mahakamani kuthibitisha ukweli kuhusu madai hayo ya kuchapisha habari za uwongo mnamo Machi 2022.

Jaji aliamuru washtakiwa ambao ni hakimu mkuu Eunice Nyuttu na Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (DPP) wakabidhiwe nakala za kesi hiyo.

Jaji Maina atatoa uamuzi ikiwa kesi hiyo ya dharau kwa mahakama itaendelea ama itafutiliwa mbali kabisa.

Mnamo Alhamisi Bi Nyuttu alimpa Bi Owuor hadi Oktoba 11, 2022 awasilishe ushahidi wake akipinga kusukumwa jela.

Bi Nyuttu alitoa agizo hilo kufuatia ombi la mawakili Assa Nyakundi, Omari na Shadrack Wamboi waliotaka mahakama iamuru wapewe ushahidi uliotolewa kortini Machi 2022.

“Tuliwasilisha ombi kwa idara ya usajili na bado hatujapewa nakala za ushahidi. Tumetumiwa ujumbe tulipie nakala hizo na tayari tumelipa,” alidokeza Nyakundi.

Mawakili hao – Nyakundi, Omari na Wamboi – waliomba hakimu awape muda ndipo wapate ushahidi huo kabla ya kuanza kumtetea mhariri Owuor.

Hakimu aliwapa muda hadi Oktoba 11 wapokee nakala za ushahidi ndipo waweze kuandaa ushahidi wa Owuor.

Owuor aliagizwa afike kortini kuadhibiwa kwa kuchapisha taarifa za kupotosha kuhusu Bi Omollo.

Mnamo Jumanne, Nyuttu alimfunga mhariri wa Tuko Didacus Malowa wiki moja alipokataa kuchapisha habari za kuomba msamaha baada ya kutuhumiwa kuchapisha habari za kupotosha kuhusu ushahidi katika kesi ya sakata hiyo ya NYS.

  • Tags

You can share this post!

Waluke ajisalimisha kwa polisi kupelekwa jela

Mjadala wapamba moto kuhusu vyakula vya GMO

T L