Habari Mseto

Mhasibu aomba aachiliwe kujiunga na mke wa wiki moja

February 21st, 2024 1 min read

NA RICHARD MUNGUTI

MHASIBU aliyekamatwa wakati wa sikukuu ya Valentino na kushtakiwa kwa wizi wa Sh39.9 milioni, aliomba mahakama imwachilie kwa dhamana amrudie mkewe aliyemuoa kabla ya sikukuu hiyo ya wapendanao.

“Naomba hii mahakama imwachilie Wyclliffe Mwangi Githinji kwa dhamana amrudie mkewe waliyekuwa wameishi naye wiki moja kabla ya polisi kumtia nguvuni,” hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Bernard Ochoi alifahamishwa na wakili anayemtetea mshtakiwa.

Bw Ochoi alielezwa kwamba mshtakiwa hakusherehekea sikukuu ya Valentino kwa vile alitiwa nguvuni Februari 14, 2024, na kuzuiliwa kwa zaidi ya saa 24 kabla ya kufikishwa kortini.

“Mshtakiwa amezuiliwa kwa zaidi ya siku tano katika kituo cha polisi kinyume na sheria inayohitaji afikishwe kortini kabla ya saa 24 kukamilika,” hakimu alielezwa.

Mahakama iliombwa imwachilie mshtakiwa amrudie mkewe “mwenye wiki moja katika ndoa.”

Mhasibu huyo alishtakiwa kwa wizi wa Sh39,904,841 kutoka kwa mwajiri wake Chemi and Cotex (K) Limited.

Bw Ochoi alielezwa na kiongozi wa mashtaka James Gachoka kwamba mshtakiwa hafai kuzua masuala kuhusu ukandamizaji wa haki zake mbele yake ila anafaa kuwasilisha hayo katika mahakama itakayosikiliza kesi hiyo ama apeleke malalamishi hayo katika Mahakama Kuu.

Akitoa uamuzi kuhusu dhamana, hakimu aliamuru mshtakiwa alipe dhamana ya pesa taslimu Sh3 milioni kabla ya kuachiliwa kutoka kizuizini.

Bw Githinji mwenye umri wa miaka 30 hakulipa dhamana hiyo, hivyo akapelekwa katika gereza la Industrial Area.

Mahakama iliambiwa alikuwa ameajiriwa na kampuni ya Chemi and Cotex (K) Limited alipotekeleza wizi huo wa Sh39,904,841.

Na wakati huo huo, mhasibu wa kampuni inayotoa huduma za ndege Joshua Kipruto Ngetich alishtakiwa kwa wizi wa Sh6.8 milioni.

Bw Ng’etich alikuwa ameajiriwa na kampuni ya African Airlines Association (AAA).

Inadaiwa Bw Ng’etich alitekeleza wizi huo kati ya Januari 2022 na Desemba 31, 2023.

Mshtakiwa alizuiliwa hadi leo Jumatano ili maafisa wa urekebishaji tabia wawasilishe ripoti kule anakoishi na ikiwa watu wa familia yake watakuwa wakimsaidia kesi inapoendelea.