HabariSiasa

#MheshimiwaFisi: Uroho wa wabunge na maseneta kukaidi kauli #PunguzaMzigo

November 22nd, 2018 3 min read

PETER MBURU Na CHARLES WASONGA

WABUNGE na maseneta wameungana kuunga mkono mswada unaopendekeza nyongeza ya marupurupu ya mamilioni na manufaa mengi licha ya wao kuwa wakitofautiana kila mara kuhusu miswada au hoja zenye manufaa kwa mwananchi wa kawaida.

Wamepuuzilia wito wa Rais Uhuru Kenyatta kwamba wakome kujiongezea mishahara na marupurupu, na badala yake wameafikiana kwa kauli moja kwamba mswada huo uharakishwe na kupitishwa mnamo Novemba 27, 2018.

Hii sasa inamaanisha wananchi watalazimika kukaza mshipi na kujinyima zaidi ili kushibisha ulafi wa wabunge na maseneta.

Mswada huo ulianza kujadiliwa bungeni jana huku wabunge wakisisitiza manufaa wanayopendekeza yanafaa kwani tayari mawaziri, makatibu wa wizara na majaji wanayapata.

Uroho wao mkubwa ulionekana wakati suala la kujenga mwafaka kuhusu Mswada wa Usawa wa Jinsia, ulioanza kujadiliwa bunge Jumanne, lilipowekwa kando na badala yake mjadala kuhusu masilahi ya wabunge ukatawala kikao hicho.

Hatua ya wabunge kuungana kwa ajili ya masilahi yao inajiri miezi miwili baada ya kugawanyika pakubwa kuhusu Mswada wa Fedha uliopendekeza nyongeza ya aina mbalimbali ya ushuru. Hatua hiyo ilisababisha kupanda kwa gharama ya maisha, hasa kwa mwananchi wenye mapato ya chini.

 

Waunganisha na ufisi

Ulafi huo umeunganisha Bunge la Kitaifa na Seneti licha ya kuwa tangu mwaka 2017 wamekuwa wakitofautiana kuhusu miswada yenye manufaa kwa umma.

Kwa mfano, mwezi Oktoba Spika Justin Muturi alimwandikia mwenzake Kenneth Lusaka barua akisema Seneti inaingilia wajibu wa Bunge la Kitaifa kwa kushughulikia mswada wa Mipaka na ule anaopendekeza kuanzishwa kwa Hazina ya Ustawi wa Wadi.

Jumanne wiki hii, wabunge wa Bunge la Taifa na Seneti wakiongozwa na maspika Muturi na Lusaka walifanya kikao ambapo waliafikiana kuharakisha kupitishwa kwa mswada ambao unapanga kuwaongezea mapato.

Mswada huo kuhusu huduma za bunge, unapendekeza kuwa wabunge wapewe nyumba bure, la sivyo wapewe marupurupu ya kulipa kodi.

Hii ni licha ya kuwa walipewa mkopo wa Sh20 milioni kila mmoja na serikali za kununua nyumba mara baada ya kuchaguliwa, hatua ambayo lengo lake ni kuhakikisha hawadai marupurupu ya kodi.

Wabunge pia wanaisukuma serikali kuwapa magari bure, na pia iwe ikiyaweka petroli, licha ya kuwa wanalipwa pesa za kuzuru maeneobunge yao kila mwezi ambazo huwa kati ya Sh266,000 na Sh444,000 kulingana na umbali wa eneo.

 

Mikopo ya mamilioni

Vilevile baada ya kuchaguliwa, wabunge hupewa mkopo wa Sh7milioni na serikali kununua gari la kikazi ambao wanalipa kwa riba ya chini katika kipindi cha miaka mitano, mbali na Sh5 milioni ambazo hawalipi kununua gari la kibinafsi. Pia kila mbunge hulipwa Sh300,000 za kurekebisha gari kila mwezi.

Katika mswada huo ambao haukupitishiwa hatua ya kuchukua maoni ya umma, viongozi hao vilevile wanataka kutengewa bajeti na ofisi katika kila eneobunge, kando na miradi ya CDF ambayo imekuwepo.

Wabunge pia wanataka bima ghali ya matibabu ambayo wanapewa pamoja na familia zao kuboreshwa, na walio na zaidi ya mke mmoja kupewa bima za wake wa ziada.

Kulingana na Tume ya Uratibu wa Mishahara ya wafanyakazi wa umma (SRC), kila afisa wa serikali na utumishi wa umma anapewa bima pamoja na mke mmoja na watoto wanne walio chini ya miaka 25.

Bima hiyo kwa wabunge huwa Sh10 milioni kwa matibabu ya kulazwa, Sh300,000 kwa matibabu na kawaida, Sh150,000 kwa huduma za mataneti na Sh75,000 kwa matibabu ya meno.

 

‘Chakula cha kitoto’

Pia wamelalamika kuhusu ‘chakula cha kitoto ‘wanachopata kwenye mkahawa bungeni, na sasa wanataka kiwe kikitayarishwa na wapishi wa hoteli za kifahari aina ya Five Star, waletewe vibuyu vikubwa vya chai na wajengewe baa ya kifahari kwa ajili ya kujiburudisha.

Kwa sasa, kila mbunge hulipwa mshahara wa Sh621,250 kila mwezi bila marupurupu. Vilevile hupata marupurupu ya usafiri wa ndani na nje ya nchi na ya kuhudhuria vikao vya kamati za bunge.

Wanapougua, viongozi hawa pamoja na familia zao hutibiwa katika hospitali za kifahari ndani na nje ya nchi kwa gharama ya mlipa ushuru, wakati walipa ushuru wengi wanapoaga dunia kutokana na huduma mbovu katika sekta ya afya.

Katika kutetea ulafi wao, wabunge wanasema kuwa wanataka kupewa huduma za hadhi kama wanazopewa mawaziri na majaji.

Hatua hii inatoa picha ya ushindani kati ya idara za serikali kuhusu ni nani atakayekula pesa nyingi zaidi za mwananchi, licha ya kuwa uchumi wa Kenya hauko imara kwa sasa.

Bajeti ya bunge katika kipindi cha mwaka wa fedha 2018/2019 ni Sh32 bilioni, ambazo zitaongezeka endapo mswada huo utapitishwa.

Hii ni kwa kuwa mbali na mapendekezo mapya waliyo nayo, bado viongozi hao wanataka kuongezewa mapato katika marupurupu ya usafiri wa humu nchini na wa kimataifa na kupewa paspoti za kidiplomasia.