Kimataifa

Mhubiri adai amemuua shetani

June 20th, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

MHUBIRI mtatanishi kutoka Afrika Kusini Paseka Motsoeneng ambaye anajulikana sana kama Nabii Mboro ameibuka na madai mapya na ya kutoaminika, akisema amekutana na shetani na akamuua.

Kupitia chapisho katika akaunti yake ya Facebook ambalo aliweka kisha akalifuta baada ya kukashifiwa, pasta huyo alidai kuwa mungu alimtuma jehonamu akammalize shetani, akisema ndiye adui mkubwa wa dunia.

“Nilipofika jehanamu, kulikuwa na foleni ya mamilioni ya watu waliokuwa wakisubiri kuitwa na shetani. Niliwaona baadhi ya wanasiasa maarufu wa Afrika Kusini. Nilishtuka sana kwa kuwa waliishi kama malaika humu duniani na nilidhani walienda mbinguni,” akasema mhubiri huyo.

“Shetani aliponiona, alishtuka na akaamrisha jeshi lake liniue. Kama Samson katika biblia, niliwashinda. Nilimuua shetani akiwa wa mwisho,” akasema.

Si mara ya kwanza kwa mhubiri huyo kuja na madai yasiyo ya kuaminika kwani mbeleni amewahi kudai kuwa alizuru mbinguni na akapiga picha aina ya ‘Selfie’ na malaika.