Dondoo

Mhubiri afumaniwa akitafuna kondoo mjini, ang'atwa sikio

February 15th, 2018 1 min read

Na CORNELIUS MUTISYA

MACHAKOS MJINI

KIOJA kilishuhudiwa katika klabu mjini hapa pasta maarufu alipong’atwa sikio na mume wa muumini wake alipomfumania akimkumbatia mkewe.

Kulingana na mdokezi, mtu wa Mungu aliwahadaa waumini wake kuwa alikuwa amealikwa mjini hapa kuhudhuria mkutano wa wahubiri. Inasemekana waumini walijitolea kumchangia pesa ili kufanikisha ziara yake.

“Pasta alichangiwa hela za usafiri na malazi na waumini wake ili ahudhurie mkutano huo. Baadhi yao waliamini kwamba kwa kumsaisdia pasta wao kueneza injili wangepata baraka,’’ alisema mdokezi.

Inasemekana kwamba, polo aliabiri gari hadi mjini hapa na akajitoma katika chumba kimoja cha starehe na kuagiza soda baridi. Alimpigia simu mwanamke aliye muumini wa kanisa lake aliyekuwa muuzaji wa mboga na matunda katika soko mjini ili wakutane waponde raha.

“Pasta alimuita muumini wake wa kike na wakaanza kupiga gumzo,’’ akasema mdokezi.

Twaarifiwa kwamba, mume wa mama huyo alipigiwa simu na jirani yake aliyewaona wakibarizi chumbani humo huku wakipapasana na kukumbatiana kimahaba.

“Mume wa mwanamke huyo alifika mara moja na akawafumania peupe wakiwa katika hali ya kutatanisha,’’ alieleza mdaku wetu.

 

Ang’atwa sikio

Duru za kuaminika zaarifu kuwa, mume wa mama huyo alimparamia pasta mithili ya simba marara na akamng’ata sikio kwa hasira. Mkewe alitoroka kupitia mlango wa nyuma alipoona mambo yamechacha.

Kulingana na mdokezi, wawili hao walitenganishwa na wahudumu wa klabu waliposikia pasta akigwaya kwa maumivu.

Walimuonya Mtu wa Mungu dhidi ya kuwanyemelea wanawake wa wenyewe na msamaria mwema akampeleka hospitali ya kibinafsi kutibiwa.