Habari Mseto

Mhubiri aliyeshtakiwa kwa wizi wa hundi ageuza mahakama 'ukumbi wa mahubiri'

June 8th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA ya Milimani Nairobi, Ijumaa iligeuzwa ukumbi wa maombi na mhubiri aliyeshtakiwa kwa wizi akidai “pepo mbaya anataka kuangamiza wito wake wa kuyahubiria mataifa.”

Huku akimshawishi hakimu mwandamizi Bi Martha Mutuku amwachilia huru bila ya kumtaka awasilishe dhamana yoyote, Steve Gordon Ochieng alisema, “Mimi ni Mtumishi wa Mungu aliye hai na kamwe siwezi kuiba maana neno la Mungu Mtukufu linanikataza kuiba.”

Mhubiri huyu aliendelea kueleza mahakama jinsi aliitikia wito wa kuachana na mambo ya ulimwengu na kuwahubiri mataifa watoroke ghadhabu ya Mungu.

“Kama mtumishi wa Mungu niliyekombolewa kutoka kwa tamaa za mwili huu, kazi yangu ni kueneza neno la Mungu watu waponye nafsi zao na ‘ziwa la moto’. Walionishtaki wameniaibisha lakini najua hii ni kazi ya Ibilisi na kundi la malaika waasi waliotoroka mbinguni kuangamiza ulimwengu,” akasema Ochieng.

Aliendelea kusimulia mahakama: “Shetani yuko na mpango wa kusambaratisha na kuangamiza kanisa langu kwa kunisingizia nimeiba lakini hatafua dafu.”

Mshtakiwa alimsihi hakimu amwachilie huru ndipo awakusanye wote waliomsingizia ameiba na kuwafikisha kortini kumnusuru.

Ochieng alisema aliitwa afike katika Benki ya Kenya Commercial (KCB) na hatimaye akaelezwa aende Benki ya Equity (EBL) kupokea pesa.

“Niliwekewa mtego mkali na nikanaswa lakini waliofanya hivyo watajua ninamtumikia Mungu aliye hai,” alisema mshtakiwa.

‘Adui huyo wa shetani na milki yake’ aliomba mahakama imwachilie kwa dhamana “arudie jamii yake sawia na kutunza kondoo wa Mungu anaowalisha kwa neno lake.”

Akimwachilia kwa dhamana, Bi Mutuku alimweleza kwamba “utapewa fursa ya kujitetea kesi itakapoanza kusikizwa Julai 19, 2019.”

Alimtaka Ochieng alipe dhamana ya pesa tasilimu Sh50,000 ama awasilishe mdhamini wa Sh100,000.

Kiongozi wa mashtaka Bi Pamellah Avedi alieleza mahakama mshtakiwa aliiba hundi ya benki ya Equity ya thamani ya Sh200 mnamo Machi 26 mtaani Runda Nairobi.

Shtaka la pili lilidai mnamo Juni 6, 2019 alijaribu kuiba Sh880,000 katika benki ya EBL tawi la Eastleigh, Nairobi.