Habari

Mhubiri anayelindwa kama Rais

December 29th, 2018 2 min read

Na MAGDALENE WANJA

SHUGHULI za kawaida zilitatizika Ijumaa mjini Nakuru wakati mhubiri wa kanisa la Repentance and Holiness Ministries David Owuor alipowasili chini ya ulinzi mkali kama unaopewa Rais Uhuru Kenyatta, uliohusisha walinzi wa kibinafsi na maafisa wa polisi waliokuwa na silaha kali.

Kuwasili kwake kuliwashangaza wakazi wa Nakuru kutokana na wingi wa magari yaliyokuwa kwenye msafara wake, mengi ya polisi sawa na yale husindikiza Rais Kenyatta, polisi wenye sare na waliovaa kiraia ambao walikuwa wakilinda doria.

Msafara mkubwa wa magari ya kifahari yakiwemo V8, Range Rover, Lexus, Prado na Mercedes ndio ulikuwa ishara yake kuingia, kukiwa na magari takriban 40 ambayo yalifululiza barabarani bila msongamano wa magari mengine.

Msafara huo uliongozwa na pikipiki za polisi sawa na zile huongoza msafara wa Rais anapohudhuria hafla za serikali.

Maafisa wa polisi wenye silaha walijaa barabarani kuzuia watu wasimtatize “nabii” huyo, huku magari manane ya polisi yaliyojaa maafisa wa kulinda usalama yakiandamana na gari lake.

Pia magari mengine yaliyokuwa na vifaa vya usalama, pamoja na hayo ya polisi yalizingira magari mawili yanayofanana na ambayo ‘nabii’ huyo aliaminika kuwa ndani ya moja yazo.

Waumini wa kanisa lake walivumilia mvua kubwa iliyowanyeshea walipokuwa wakimsubiri, japo iliwasaidia kuepuka kazi ya kumuoshea barabara jinsi wamekuwa wakifanya kila anapozuru mji huo.

Shughuli hizo zilitatiza usafiri katika barabara kuu ya Nairobi-Nakuru na nyingine za kati ya mji wa Nakuru, kwani waumini walikuwa wamejazana na kuziba barabara, wasafiri wakilazimika kutumia njia mbadala.

Alipowasili, ‘nabii’ huyo alikaribishwa kwa nyimbo na nderemo na wafuasi wake waliolowa maji, naye aliposhuka kwenye gari lake la kifahari akawahutubia kidogo kwa kuwakumbusha ‘miujiza’ aliyowahi kuwafanyia mbeleni na kuwaita mbele watu ambao aliodai kuwatendea miujiza hiyo.

Si mara ya kwanza kwa ‘nabii’ huyo kupewa ulinzi mzito kiwango hicho, kiasi cha kuwaacha watu midomo wazi, wengine wakishangaa sababu huwa nini na hali kulingana na imani ya Kikristo ulinzi wake umehakikishwa na Mungu.

Katika mikutano ya mbeleni na wafuasi wake haswa mmoja aliofanya katika bustani ya Uhuru Park jijini Nairobi, aliwasili kwa ulinzi kama wa Rais, kwani alikuwa akilindwa vikali na maafisa wa polisi.

Polisi waliokuwa wakilinda gari lake walijihami kwa silaha na hata magwanda ya kujikinga kutokana na risasi.

Anaposhuka kwenye gari lake anapohubiri, “nabii” huyo huwa anatandikiwa zulia jekundu kama la marais na wafalme hadi kwenye ‘madhabahu’.

Aidha, wakati mmoja alipozuru jijini Nairobi na kuhubiria watu barabarani, alikuwa na magari ya kifahari na walinzi wenye suti ambao walikuwa na vifaa vya mawasiliano ya walinda usalama, wakizuia watu waliokaribia magari yake ama ‘nabii’ huyo.

Anapokuwa jukwaani, walinzi waliovalia suti kama wale wa rais huwa wamelizingira kiasi kwamba hakuna mtu anayeweza kuwapita huku macho yao yakiwa wazi kila dakika kwa maelfu ya waumini ambao hufurika.

Mkutano anaohudhuria mjini Nakuru, ambao umepewa jina ‘Grand Mega Healing’ (hafla kubwa ya uponyaji) utaandaliwa katika bustani ya Menengai, ambapo maelfu ya wafuasi wake wanatarajiwa kuhudhuria.