Habari

Mhubiri wa SDA akatakata mke wa ndugu yake

July 23rd, 2019 2 min read

Na NDUNGU GACHANE

POLISI katika Kaunti ya Murang’a wanamsaka mhubiri wa kanisa la SDA, ambaye alimvamia shemeji yake na kumkatakata kwa upanga.

Mhubiri huyo, ambaye anaishi na kuhudumu jijini Nairobi, alimpigia simu mmoja wa wanawe wa kiume mnamo Jumatatu na akamfahamisha kuwa alikuwa safarini kuelekea nyumbani kwao katika kijiji cha Gikomora, Maragua, na kuwa angewaua watu wote wa familia yake.

Mwanawe, hata hivyo, alimfahamisha mamake na wakatoroka kujiokoa kabla ya mhubiri huyo kufika.

Alipofika na kuwakosa, aliamua kumwangushia hasira shemeji yake kwa jina Felister Njoki kwa kumkatakata shingoni, mikononi, mgongoni na kichwani.

Mkazi ambaye hakutaka kutajwa, alisema mshukiwa alimvamia Bi Njoki alipokuwa akifanya kazi katika boma asubuhi ya Jumanne.

“Alikatwa shingoni, mgongo, mikononi na kichwani. Tulipofika tulimpata akiwa amezirai, huku damu ikiwa imetapakaa. Hatukuamini kuwa mhubiri anaweza kufanya hivyo kwa kuwa tunajua huwa anahubiri Nairobi,” akasema mkazi huyo.

Iliwabidi wakazi kuingilia kati kumuokoa mwathiriwa na wakamkimbiza katika hospitali ya Maragua Level 4 akiwa amepoteza fahamu kutokana na majeraha mengi ambayo alikuwa amepata, pamoja na kupoteza damu.

Wakazi walisema mhubiri huyo amekuwa akionyesha dalili za kutokuwa katika hali nzuri ya kimawazo, wakisema mbeleni kuna wakati alijaribu kujiua, lakini jaribio lake likagonga mwamba.

Afisa msimamizi wa hospitali ya Kaunti ya Murang’a, Leonard Gikera alisema Bi Njoki alihamishwa hadi hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta kwa matibabu zaidi.

“Alikuwa na majeraha ya kukatwa sana katika sehemu tofauti za mwili, lakini tuliweza kumpa dawa za kumsaidia kabla ya kumtuma katika hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta kwa matibabu maalum,” akasema Dkt Gikera.

Kisa hicho kilitokea wakati Kaunti ya Murang’a siku za majuzi imekuwa ikishuhudia visa vya fujo za kinyumbani, hali ambayo imelaumiwa kwa matumizi ya bangi.

Mkuu wa Polisi wa Murang’a Kusini, John Ondit alisema kuwa polisi wameanzisha msako dhidi ya mshukiwa huyo, ambaye anaaminika alitorokea Nairobi baada ya kutenda unyama huo.

“Alitorokea Nairobi baada ya kumkatakata mjane huyo wa ndugu yake lakini tutamkamata,” akasema Bw Ondit.