Mhudumu wa bodaboda anusurika kifo kwa kichapo

Mhudumu wa bodaboda anusurika kifo kwa kichapo

NA WYCLIFFE NYABERI

Maafisa wa polisi katika kaunti ya Nyamira jana walilazimika kufyatua risasi hewani ili kumuokoa mhudumu mmoja wa bodaboda aliyekuwa akipigwa na wenzake kwa kosa la kumuibia mteja wake zaidi ya Sh 100, 000.

Bw Benard Obwoge, anasemekana kumuibia mwanamke anayehudumu kwenye duka la Mpesa sokoni Kebirigo baada ya kumbeba kutoka sehemu za Rirumi.

Mfanyabiashara huyo aliyekuwa na mtoto, alimpa bodaboda huyo kipochi chake ambebee ndiposa apate nafasi nzuri ya kumkinga mwanawe kutokana na baridi kali anayohisi mtu anayesafiria pikipiki lakini jamaa huyo alifungua kibeti hicho na kukwachua hela zake.

Mama huyo alipigwa na butwaa aliposhukishwa na kuona begi lake limefunguliwa.Bila kusita, mwanamke huyo alipiga kamsa iliyowavutia wanabodaboda wengine waliomfuata alikotorokea jamaa huyo.Bodaboda hao walimkamata na kumrudisha Kebirigo na kuanza kumdhuru lakini maafisa wa polisi wakasambaratisha kupigwa kwake kwa kuwatawanya na risasi za hewani.

Hata hivyo, pesa za mama huyo hazikupatikana kwani inasemekana bodaboda waliomfukuza mwenzake na kumkuta nazo walijitunuku kwa kuzigawanya miongoni mwao.Baadhi ya wahudumu hao walikamatwa ili kuelezea jinsi pesa za mama huyo zilipotea.

Katika tukio tofauti jana, wakazi waliokuwa na ghadhabu katika eneo la Kijauri walipania kumteketeza mshukiwa mwingine wa mbuzi lakini akaokolewa na msamaria mwema aliyekuwa akipita na gari lake.Mbuzi hao watatu walisemekana kuibwa kutoka mojawapo ya sehemu za Nyansiongo lakini jamaa huyo akawahiwa.

Polisi wanamzuilia mshukiwa uchunguzi ukianzishwa.Kutokana na visa hivyo, kamanda wa polisi katika kaunti ya Nyamira Bi Catherine Mugwe amewaomba raia kutojichukulia sheria mikononi mwao bali kuwasilisha washukiwa wowote kwa polisi ili hatua mwafaka zichukuliwe.

  • Tags

You can share this post!

Copa America kung’oa nanga leo usiku

Magavana tumbototo kuhusu miradi waliyoanza