Habari

Mhudumu wa mochari alilia korti aendelee kuvuta bangi

January 3rd, 2020 2 min read

Na BRIAN OCHARO

MWANAMUME alidai mahakamani kuwa mfanyakazi wa mochari, Alhamisi aliomba korti imruhusu aendelee kuvuta bangi, akisema humsaidia kufukuza mapepo.

John Thuranira Kaberia ambaye alidai anafanya kazi katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali Kuu ya Pwani, alisema bangi humsaidia kufukuza mapepo ambayo humuandama akiwa chumbani kwake usiku.

“Napata wakati mgumu sana usiku, silali kwa sababu nakesha nikiona sura za maiti zikinijia usoni. Jambo hili linanishtua sana na kunifanya nikose usingizi,” akasema Bw Kaberia.

Mshukiwa huo ambaye anakabiliwa na shtaka la kupatikana na mihadarati hiyo alisema kuwa kazi hiyo inampa shida sana, hasa wakati wa usiku na kuwa hali hiyo imemkosanisha na mkewe.

“Ninakosana na mke wangu kila siku hasa wakati tukienda kanisani. Ananikasirikia kuwa mimi ni mcha Mungu na kwa upande mwingine ninavuta bangi. Tumekuwa na mtafaruku katika uhusiano wetu,” aliambia Hakimu Mwandamizi Mkuu Martin Rebera.

Pia, Bw Kaberia alisema kutokana na kazi yake ya kuhudumia maiti, amekosa hamu ya kula chakula na kuwa bangi imekuwa ikimsaidia kurejesha hamu ya kula.

“Nikivuta bangi ninapata hamu ya kula na chakula kinateremka vizuri; si kupenda kwangu lakini hali yangu imenilazimu nivute bangi,” aliongezea.

Mshukiwa alisema kabla ya kukamatwa, alikuwa katika harakati ya kutafuta kibali kutoka kwa polisi kuendelea kuvuta bangi ili asitatizike na kushtuliwa na sura za maiti.

Hata hivyo, Bw Rabera alimshauri mshukiwa kuwa akitaka kuendelea kuvuta bangi bila kusumbuliwa, ni sharti atafute kibali kutoka kwa polisi na karatasi kutoka kwa daktari ambayo inamkubalia kutumia mihadarati hiyo.

“Hata sisi vile vile tunafanya kazi ngumu lakini hatutumii bangi, lakini kama unataka kuendela kutumia mihadarati hiyo, ni lazima upate kibali ambacho utapatiwa baada ya kuwasilisha barua kutoka kwa daktari,” Bw Rabera alimshauri.

Katika karatasi ya mashtaka, Bw Kaberia alishtakiwa kwa kupatikana na misokoto minne ya bangi.

Mahakama iliambiwa kuwa mshukiwa huyo alipatikana na mihadarati hiyo , ambayo ilikuwa ya thamani ya Sh100.

Bw Kaberia alikubali kosa hilo ambalo polisi walisema alifanya mnamo Desemba 31, 2019, katika eneo la Ferry, kwenye kaunti ndogo ya Likoni.

Kesi hiyo itatajwa Januari 13 kwa maagizo zaidi.