Habari Mseto

Mhudumu wa zamani akamatwa kwa ‘kusumbua’ maiti mochari

October 31st, 2020 1 min read

Na Evans Kipkura

MAAFISA wa usalama katika Hospitali ya Rufaa ya Iten, Kaunti ya Elgeyo-Marakwet, Jumatano walimkamata mhudumu wa zamani wa mochari katika hospitali hiyo kwa tuhuma za kuharibu miili iliyohifadhiwa humo.

Inadaiwa mshukiwa, ambaye alitambuliwa kama Benson Kagari, aliingia katika mochari Jumatano usiku bila kugunduliwa na yeyote.

Kwenye taarifa, Waziri wa Afya katika kaunti hiyo, Bw Isaac Kamar, alisema mshukiwa aliingia katika mochari kupitia dirishani na kwenda moja kwa moja hadi eneo ambako miili inawekwa.

“Tulipokea ripoti kwamba kulikuwa na mtu aliyeingia kwenye mochari ambapo alikuwa akiharibu miili iliyohifadhiwa na kuibadilisha ili kuwachanganya wahudumu.Tulifika kwa haraka na kubaini kuwa ni mhudumu wa zamani aliyefutwa kazi kutokana na utovu wa nidhamu,” akasema Bw Kamar.

Waziri alisema kuwa maafisa hao waliingia kwenye mochari hiyo kwa haraka na kumkamata mshukiwa, ambapo baadaye walimkabidhi kwa polisi ili kuchunguzwa.

Alisema kuna uwezekano mshukiwa alitumiwa na baadhi ya watu kuwapaka tope wafanyakazi katika taasisi hiyo kama wasiojali.