Makala

Miaka 10 baadaye, soko la Free Area, Nakuru halijakamilika

September 15th, 2019 3 min read

NA RICHARD MAOSI

SOKO aliloanzisha Rais Uhuru Kenyatta akiwa waziri wa fedha mnamo 2009, katika eneo la Free Area, Kaunti ya Nakuru, miaka 10 baadaye halijakamilika.

Ni kwa sababu hiyo wanunuzi wamekuwa wakijitenga na soko hilo kubwa huku wakiacha bidhaa za wauzaji zikibaki kuharibika.

Taifa Leo Dijitali ilibaini njia hazipitiki kutokana na matope mengi, hasa wakati huu wa mvua ambapo hali ya miundo msingi imebaki kuwa duni.

Soko la Freearea ni miongoni mwa masoko kongwe yaliyoanzishwa katika maeneo bunge 210 kote nchini kupitia mradi wa Stimulus Fund, ambapo kila sehemu ilitengewa milioni 10 kwa ajili ya ukarabati.

Kulingana na msimamizi wa wafanyibiashara Allan Omahe,alisema soko limetengenezewa ukuta hafifu na kuzungushiwa waya,jambo linalofanya mbuzi na kondoo kuwaibia wafanyibiashara bidhaa zao.

Aidha wafanyibiashara wengi wanaona ni afadhali kujiundia vibanda vya muda kuendeshea biashara zao kwa sababu soko ni chafu wala halina vyoo.

Allan anasema wale waliopaswa kufaidika na mradi wa Stimulus Fund waibadilisha kazi kwa sababu waliishi kwa muda mrefu wakisubiri soko la kisasa litamatike.

“Wengine wao walikata tamaa na kugeukia masoko kwingine baada ya serikali kuu kutoonyesha dalili ya kuwaboreshea mazingira ua kuuzia,” akasema.

Baadhi ya wauzaji wanaochuuza bidhaa zao juu ya mawe katika soko la Gilgil kaunti ya Nakuru,wanasema wamekuwa wakichomwa na jua. Picha/ Richard Maosi

Allan anashindwa endapo ni utepetevu wa mkandarasi au fedha zilizotengewa mradi huo zilifujwa kabla ya mradi kung’oa nanga..

Anaongezea kuwa wakati wa serikali ya ugatuzi,sehemu ya paa ilimalizika,na hata sehemu za kuweka mizigo kutengenezwa.

Kwenye bajeti ya 2017-2018 alifikiri mradi huo ungemalizika kwa sababu kazi ilipatiwa mkandarasi mpya ambaye aliendeleza ujenzi lakini akakomea njiani.

Anasema wauzaji wengi wameshakata tamaa na badala yake kujitengenezea vibanda kando ya barabara, akisema ni bora kuliko jengo lililotengenezwa na serikali kuu lakini sasa ni mahame.

Soko la Freearea mjini Nakuru ambapo mbuzi huingilia maeneo ya biashara na kuwaibia mboga na matunda. Picha/ Richard Maosi

Anasema soko jipya limetengenezewa tu sakafu na wala hakuna jambo jingine kubwa ambalo wauzaji wanaweza kujivunia.

“Nyanya ,vitunguu na sukuma wiki zinahitaji kutengewa sehemu maalum ya kuhifadhiwa,” akasema.

Alisema kuwa kwanza ni lazima serikali ya ugatuzi iboreshe hali ya soko ili kuwapatia wafanyibiashara ujasiri wa kufanya kazi.

Kulingana naye mazingira safi na salama ndio huvutia wateja wengi,na yanaweza kutengeneza ajira kwa vijana wengi wanaoshinda mitaani.

Bi Margret Waithera mama ya watoto watatu, anasema amekuwa akifanya kazi ya uuzaji kwa mboga takriban miaka kumi sasa.

Hii ni mirundiko ya taka inayotupwa ovyo katika soko la Freearea inayopatikana kilomita chache kutoka Nakuru. Picha/ Richard Maosi

Anasema soko kubwa kama hili linahitaji maji ya mfereji ili kuwauzia wateja matunda na mboga safi.Kwake yeye mkurupuko wa maradhi ni jambo la kawaida.

Aliongezea tangu viongozi waingie mamlakani hawajawahi kuonekana Freeatea isipokuwa utawala wa kaunti uliopita ambapo Kinuthia Mbugua aliwatembelea wauzaji mara moja tu..

Anasema kuwa alisikia kuwa ni mkandarasi wa kichina alipatiwa kandarasi ya kutengeneza soko hadi hatua ya mwisho.

Lakini hali imebaki kuwa vilevile wafanyibiashara wakilazimika kusubiri kwa muda mrefu zaidi.

Barabara ya kuelekea katika soko ni mbaya na haipitiki hasa msimu huu wa mvua nyingi. Picha/ Richard Maosi

Anasema wamekuwa wakijadiliana na viongozi wa kaunti katika mikutano wa hadhira lakini pindi waondokapo malalamishi yao hutupiliwa mbali katika kaburi la sahau.

Taifa Leo dijitali ilishuhudia baadhi ya mbuzi na kondoo wakiwapokonya wauzaji bidhaa zao,kulingana nao imekuwa ni desturi.

Wafanyibiashara kwenye soko la Kiamunyeki,Kaptembwa Nasha,Gilgil na Freearea walieleza Taifa Leo dijitali kuwa wakati mwingi wao hulazimika kupigana na mifugo wanaoingia sokoni kuwapokonya bidhaa.

Ni katika hali hiyo serikali ya kaunti ya Nakuru hivi karibuni, imeanzisha mikakati ya kufufua baadhi ya mijengo ambayo mpaka sasa haifanyi kazi.

Soko la Freearea halina ukuta isipokuwa waya hafifu uliozungushwa na hali yenyewe haijawahakikishia wauzaji usalama kwa bidhaa zao. Picha/ Richard Maosi

Ingawa utawala wa gavana Kinuthia Mbugua unanyoshewa kidole cha lawama kwa sababu ya mazingira duni sokoni, uchelewaji wa kutengeneza soko la kisasa ni jambo jingine.

Katikati ya mji wa Nakuru serikali ilitoa kima cha shilingi milioni 20 kukarabati soko la Wakulima,Waliunganishiwa taa za umeme na maji ya mfereji.

Ingawa baadhi yao wameridhika,bado utepetevu katika uzoa takataka ni jambo la kutiliwa shaka, angalau shughuli hapo zinaendeshwa kwa mpngilio maalum.

Aidha baadhi ya wafanyibiashara wanahangaishwa na jua kila siku au mvua kuwanyeshea hasa wakati huu ambapo mvua imeanza.

Hii ni milango ya baadhi ya vyoo katika soko la kisasa Freearea ambayo ilitengewa milioni 10 kutengenezwa. Picha/Richard Maosi

“Wakati wa mvua nyingi barabara haziwezi kupitika,na pia kuna magenge ya wahalifu yanayowahangaisha wateja wakati wa giza,”Rebecca Nandwa mfanyibiashara mwingine alitufichulia.

Hata hivyo vijana wengi wanaofanya kazi za uchukuzi beba wanasema itakua ni afueni ikiwa soko zitaboreshwa ili kuwasaidia watengenezea nafasi za kazi.

Katika sehemu zingine kama Kaptembwa na Pondamali wafanyibiashara wamekuwa wakianika bidhaa zao juu ya mawe wakisema ni safi kuliko vibanda vya kisasa.

“Hakuna mabadiliko makubwa katika soko za kisasa isipokuwa sakafu ya saruji na paa la bei ghali,” Bi Rebecca alisema.

Huenda ndio sababu baadhi ya wakulima wanaona ni bora kujitengenezea vibanda vya kuhamahama badala ya kutegemea serikali ya ugatuzi ambayo imewatenga.

Miongoni mwa mambo mengine ambayo wafanyibiashara wanaomba kurekebishiwa ni pamoja na kutengenezewa barabara la lami,kuimarishwa kwa usalama,vyoo na maji safi ya mfereji.

Awamu ya uongozi ni wa kulaumiwa kwani serikali zote zilizotangulia zimekuwa zikitumia hali mbaya ya soko la Freearea kujipigia debe.