Makala

Miaka 30 ya balaa tupu: Simulizi za vijana watatu walivyokaribisha umri ‘unaoogopwa’

April 19th, 2024 2 min read

NA FRIDAH OKACHI

MIAKA ya thelathini katika maisha huwa yenye hisia tofauti. Kufikisha umri wa miaka 30 kwa wengine huwa jambo la kupendeza au kutamausha.

James Kaburu, 38, anaishi na uchungu, safari ya maisha yake ikikosa kuwa na mabadiliko. Alipokuwa na umri wa miaka ishirini, alikuwa na matumaini ya kukutana na mambo ya kupendeza, kuona ulimwengu na kufurahia. Lakini sivyo yalivyo, na ameapa kutosherehekea siku yake ya kuzaliwa kutokana na changanoto za maisha zinazomkabili.

“Nasherekea kufikisha umrei wa miaka 39 mwezi huu. Sina kazi, sina nyumba, sina gari na sipo kwenye mahusiano. Umri wangu ni mkubwa, kwa hivyo sina chochote cha kujivunia. Na ndio sababu huwa sisherekei siku yangu ya kuzaliwa,” anasema Kaburu.

Akiwa na shahada ya ualimu, amesalia kufanya kazi katika shule za binafsi, malipo yakiwa duni.

“Mshahara ninaopata ni wa kulipa nyumba na kushughulikia mahitaji yangu ya kila siku. Kuna kaka na dada wanaohitaji msaada wangu. Sibakii na pesa zozote,” aliongeza.

Mtaa wa Ngong, Kaunti ya Kajiado, Rama Bedia alikuwa mwenye maono makubwa na ndoto za ajabu. Baada ya kumaliza chuo kikuu akiwa na umri wa miaka 24, aliona ni vyema kufunga ndoa ili kuanza maisha, bila kufahamu yaliyomsubiri mbele yake. Amebaki kutamaushwa na jinsi mambo yalivyo na hivyo kutumia dawa za kupunguza mawazo almaarufu anti-depressant.

“Nikiwa na miaka 25, tayari nilikuwa na nyumba na gari. Miaka 30 nilikuwa na watoto wanne. Miaka 35 nilimpa mke wangu talaka na sasa maisha yangu yanategemea kumeza dawa za kupunguza mawazo mengi,” anasema Bendia.

Matatizo chungu nzima yalimkabili alipochukua mkopo ambao ulikuwa ni wa kiasi kikubwa. Mkopo huo akitumia na marafiki jambo ambalo lilimkera mke wake.

“Kiasi kidogo niliweka kwenye biashara. Pesa nyingi nilitumia na marafiki, kila wakati nilifahamu nina kazi ya kulipia. Bila kujua litakalotokea, kazi iliisha, ugomvi kati yangu na mke wangu ulizidi tukatalikiana,” alifafanua Rama.

Naye Sophia Wanja, mwenye umri wa miaka 32, amesalia kushangaa kutokana na wenzake wenye umri sawa na wake kuwa na familia. Miaka miwili iliyopita, tayari alikuwa amekata kauli kuwa hatakuwepo kutokana na maisha kuwa magumu kwake.

“Kauli ya mwaka huu, sikuwa tayari na kuhitimu miaka yangu niliyo nayo sasa. Nilijua kuwa tayari nitakuwa nimekutana na Maulana. Ila sasa najaribu kutafuta namna ya kufanya mambo ambayo nilifaa kufanya nikiwa na umri wa miaka 20,” alisema Wanja.

Mshauri nasaha Bw James Kariuki alisema miaka ya thelathini vijana wanahitaji kujituma zaidi na kuhakikisha wanatimiza maono yao.

“Wengi huanza kujitambua wakiwa na miaka 25-30. Ukihitimu miaka 30 una miaka chini ya thelathini na mitano kufanya kazi. Na unapozidi kukua unakuwa na uzoefu wa maisha na pia kuanza kuchoka,” alikamilisha Kariuki.