Michezo

Miaka 4 zaidi Dier akichezea Spurs

July 22nd, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIUNGO mkabaji wa Tottenham Hotspur, Eric Dier amerefusha mkataba wake kambini mwa miamba hao wa soka ya Uingereza hadi mwishoni mwa msimu wa 2024.

Dier, 26, aljiunga na Tottenham mnamo 2014 baada ya kuagana rasmi na kikosi cha Sporting Lisbon nchini Ureno kwa kima cha Sh560 milioni.

“Nafurahi sana kwamba nitakuwa sehemu ya kikosi kitakachotegemewa na Tottenham katika kipindi cha misimu kadhaa ijayo,” akatanguliza Dier ambaye pia ana uwezo wa kutamba akiwa beki wa kati.

“Tottenham walinipa fursa ya kudhihirisha uwezo wangu uwanjani katika soka ya Uingereza. Wamenifanyia mengi ambayo natambua na kuthamini. Ni matarajio yangu kwamba nami nitaendelea kujitahidi na kuwatambisha katika kipindi hiki ninapovalia jezi zao,” akaongeza Dier.

“Lengo langu ni kushirikiana vilivyo na kocha pamoja na wanasoka wengine ili kushindia Tottenham idadi kubwa zaidi ya mataji ya haiba kubwa. Ningependa kuondoka Tottenham nikifahamu kwamba nimefanya yote ambayo yamo ndani ya uwezo wangu katika juhudi za kuwavunia mataji muhimu ndani na nje ya kampeni za soka ya Ujerumani,” akaongeza.

Hadi kufikia sasa, Dier amewajibishwa na Tottenham katika jumla ya mechi 239 na akapachika wavuni mabao 11.

Mnamo Julai 8, 2020, Dier alipigwa marufuku ya mechi nne na kutozwa faini ya Sh5.6 milioni kwa kosa la kumvamia shabiki aliyemtusi uwanjani mnamo Machi 2020.

Tukio hilo lilitokea mwishoni mwa mechi iliyoshuhudia Tottenham wakibanduliwa na Norwich City kwenye kipute cha kuwania ubingwa wa Kombe la FA msimu huu.

Dier pia alionywa na FA kwamba atakuwa katika hatari ya kuadhibiwa vikali zaidi katika siku za usoni iwapo atarudia makosa ya sampuli hiyo.

Tukio hilo lilifanyika mnamo Machi 4 wakati wa mechi ya raundi ya tano ya Kombe la FA iliyoshuhudia mshindi akiamuliwa kwa mikwaju ya penalti. Licha ya Dier kupachika wavuni mkwaju wake, waajiri wake Tottenham walipoteza mechi hiyo na hatimaye kubanduliwa nje ya kipute cha Kombe la FA.

Wakati huo, kocha Jose Mourinho alikataa kabisa kuzungumzia suala hilo, akionya kwamba Tottenham na Dier wangalijipata katika hatari ya kuadhibiwa vikali zaidi iwapo yeye angefichua msimamo wake wa kutetea kikosi chake na matendo ya mwanasoka wake huyo.

Dier anajivunia kuvalia jezi za timu ya taifa ya Uingereza katika mechi 40 za hadi kufikia sasa.