MIAKA 40: Museveni ashinda urais kwa mara ya sita mfululizo

MIAKA 40: Museveni ashinda urais kwa mara ya sita mfululizo

Na CHARLES WASONGA

TUME ya Uchaguzi Uganda (UEC) imetangaza Rais Yoweri Kaguta Museveni kama mshindi wa uchaguzi wa urais baada ya kuzoa kura 5,851,037 kulingana na mwenyekiti wa tume hiyo Jaji Simon Byabakama.

Hii ni sawa asilimia 58.64 ya kura zote za urais zilizopigwa katika uchaguzi huo uliofanyika Alhamisi, Januari 14, 2021.

Mgombea wa chama cha upinzani cha National Unity Platform (NUP) Robert Kyagulanyi, almaarufu Bobi Wine, alizoa jumla ya kura 3,475,298. Hii ni sawa na asilimia 34.83 ya idadi jumla ya kura za urais zilizopigwa.

Bw Museveni sasa ataongoza Uganda kwa muhula wa sita mfululizo, na kufikisha miaka 40, idadi ya miaka ambayo atakuwa rais wa Uganda.

“Namtawaza Yoweri Museveni Tibuhaburwa, kuwa rais ya wa Jamhuri ya Uganda baada ya kupata kura nyingi zaifi katika uchaguzi uliofanyika Januari 14, 2021,” akasema Jaji Byabakama.

Mgombeaji wa chama cha Forum for Democratic Change (FDC) Amuriat Oboi alishikilia nambari tatu kwa kupata kura 323,536, zinazowakilisha asimilia 3.24 za kuwa ilhali wagombeaji wengine walipata chini ya asilimia moja ya kura.

Wagombeaji wengine, kama vile Mugisha Muntu wa chama cha Alliance for National Transformation alipata kura 65,334 (sawa na asilimia 0.65), Norbert Mao wa Democratic Party aliyepata kura 55,665 (asimilia 0.56) huku Joseph Kabuleta ambaye ni mgombeaji huru akipata kura 44,3000 (asilimia 0.44).

Wagombeaji wengine huru Nancy Kalembe alipata kura 37,469 (asimilia 0.38), John Katumba alipata kura  35,983 (0.36%), Willy Mayambala alipata  kura 14,657 (0.15%), Fred Mwesigye alipata kura   24,673 (0.25%) na  Henry Tumukunde akapata kura 50,141 (0.50%).

Hata hivyo, akiongeza na wanahabari awali Bw Kyagulanyi alipinga matokeo hayo yaliyotangazwa na EC akisema kulikuwa na udanganyifu katika upigaji kura na ujumuisha kura.

“Leo asubuhi jinsi mlivyoona matokeo ya awali ya tume Ya uchaguzi yanaonyesha kuwa Museveni alipata asilimia 63.92 ya kura na sisi tumepatiwa asilimia 28.32. Tunapinga matokeo hayo kwa sababu tumeona udanganyifu uliokuwa ukiendelea tangu kipindi cha kampeni, hadi upigaji kura na ujumuisha wa kura hizo,” Bw Kyangulanyi akasema Ijumaa.

Akaongeza: Maajenti wetu katika wilaya mbalimbali magharibi na kaskazini mwa Uganda haswa Magharibi mwa Nile, walikamatwa lakini EC ikaendelea kusoma matokeo bila wao kuyathibitisha. Tunaamini kuwa tumemishinda Museveni katika uchaguzi huu.”

Akijibu matokeo hayo mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi alisema madai ya Bw Kyangulanyi hayawezi kuthibitishwa.

‘Matokeo yote yaliyotangazwa yalikuwa yamethibitishwa na maajenti wa wagombeaji wote ambao walitia saini fomu maalum kutoka vituo vyote 34,684 vya kupigia kura. Mheshimiwa Kyangulanyi ana fomu hizo zote, na hivyo awaambia wananchi ni jinsi ipi udanganyifu ulitokea,” akasema Jaji Byabakama.

You can share this post!

Bruno Fernandes aweka rekodi EPL

Zifahamu faida za hiliki