Shangazi Akujibu

Miaka miwili ya ndoa nasubiri mke ashike mimba kumbe anameza tembe!

April 29th, 2024 1 min read

Shangazi;

Nimekuwa nikishangaa ni kwa nini mke wangu hapati mimba miaka miwili baada ya kumuoa. Kumbe anatumia dawa za kuzuia mimba! Ameniambia hajawa tayari kuwa mama.

Mojawapo ya sababu kuu za ndoa ni kupata watoto. Kama mke wako hana sababu nzuri ya kutopata watoto sasa, ni muhimu mzungumze ili mjue mwelekeo wa ndoa yenu.

Kuna domokaya anatishia kuniharibia ndoa

Nina mke na watoto. Kuna mwanamke anayeeneza uvumi mtaani eti sisi ni wapenzi. Sielewi nia yake hasa na nahofia udaku huo ukimfikia mke wangu atazua balaa. Nifanyeje?

Shahidi mkubwa ni ukweli. Hata habari hizo zikimfikia mkeo atafuatilia na kujua ukweli. Lakini ni muhimu umtafute mwanamke huyo ili ujue nia yake na kumuonya akome kueneza uvumi huo.

Ndugu yangu amepita na shemeji ghafla

Vipi shangazi? Ninaendelea na mipango ya kufunga ndoa na barafu wa moyo wangu. Lakini ndugu yangu amependana na dada yake na wameoana ghafla. Hatua yao hiyo imenichanganya. Nifanye nini?

Kila jamii ina tamaduni zake. Jamii nyingi zinaruhusu wanaume ndugu kuoa kutoka familia moja. Tafuteni ushauri kutoka kwa jamaa zenu ili mpate mwelekeo.

Nitalemewa kulea wana wa Ex pamoja na wetu

Hujambo Shangazi. Mpenzi wangu ana miaka 35 nami nina 27. Nampenda kwa dhati na nataka kumuoa. Lakini ana watoto wawili kutokana na uhusiano wa zamani. Ninahisi watakuwa mzigo kwangu kulea tukizaa wengine.

Kuna mambo unayofaa kuzingatia kabla ya kufunga ndoa ili kuepuka majuto baadaye maishani. Unafaa kupata watoto kulingana na uwezo wako wa kulea. Usijitwike mzigo usioweza kubeba.