Michezo

Miamba Algeria waponea chupuchupu kinywani mwa Burkina Faso

January 20th, 2024 1 min read

Na MASHIRIKA

BAO la dakika za mwisho kutoka kwa Baghdad Bounedjah liliwazolea miamba Algeria pointi ya pili katika Kundi D kwenye fainali za Kombe la Afrika (Afcon) baada ya kuambulia sare ya 2-2 dhidi ya Burkina Faso.

Mohamed Konate aliwaweka Burkina Faso almaarufu Stallions kifua mbele mwishoni mwa kipindi cha kwanza kabla ya juhudi zake kufutwa na Bounedjah aliyesawazisha mambo mwanzoni mwa kipindi cha pili.

Ingawa Bertrand Traore alirejesha Burkina Faso uongozini kupitia penalti ya dakika ya 71, Algeria ambao ni wafalme mara mbili wa Afcon walijituma maradufu hadi wakaondoka uwanjani na alama moja muhimu.

Matokeo hayo yaliacha Burkina Faso na alama nne sawa na Angola waliopepeta Mauritania 3-2 katika pambano jingine la Kundi D, Jumamosi.

Algeria walioibuka mabingwa wa Afcon mnamo 2019, wanakodolea macho hatari ya kudenguliwa mapema au kulazimika kusubiri kuona iwapo watakuwa miongoni mwa vikosi vinne bora vitakavyomaliza kampeni za makundi katika nafasi za tatu iwapo watashindwa kuangusha Mauritania katika pambano lao lijalo mnamo Januari 23, 2024.

Burkina Faso walipoteza nafasi nyingi za kufunga kupitia kwa Steeve Yago aliyeshirikiana vilivyo na Blati Toure. Penalti waliyofungiwa na Traore lilitokana na tukio la Rayan Ait-Nouri kumchezea Issa Kabore visivyo ndani ya kijisanduku.

Burkina Faso watafunga kampeni zao za Kundi D kwa gozi kali dhidi ya Angola mnamo Jumanne.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO