Miamba Atletico Madrid watolewa mapema kwenye kivumbi cha Copa del Rey

Miamba Atletico Madrid watolewa mapema kwenye kivumbi cha Copa del Rey

Na MASHIRIKA

VIONGOZI wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), Atletico Madrid waliduwazwa na limbukeni UE Cornella ambao waliwapokeza kichapo cha 1-0 kilichowabandua kwenye raundi ya pili ya kampeni za kuwania taji la Copa del Rey msimu huu wa 2020-21.

Adrian Jimenez aliwafungia UE Cornella bao la pekee na la ushindi kwenye mechi hiyo katika dakika ya saba alipokamilisha kwa ustadi krosi aliyopokezwa na Agustin Medina. Cornella hushiriki soka ya Ligi ya Daraja la Tatu nchini Uhispania.

Chini ya kocha Diego Simeone, Atletico walijipata wakicheza mechi 27 za mwisho wa mchuano huo wakiwa na wachezaji 10 pekee ugani baada ya Ricard Sanchez kuonyeshwa kadi nyekundu baada ya makosa mawili yaliyompa kadi mbili za manjano.

Pigo kubwa zaidi kwa Atletico ambao kwa sasa wanaongoza jedwali la La Liga kwa alama 38, ni jeraha la kifundo cha mguu litakalomweka nje beki matata Jose Gimenez.

Huu ni msimu wa pili mfululizo ambapo Atletico wamebanduliwa mapema kwenye soka ya Copa del Rey na kikosi cha Ligi ya Daraja la Tatu nchini Uhispania. Mnamo 2019-20, miamba hao walidenguliwa na Cultural Leonesa.

You can share this post!

Man-City kuvaana na Spurs kwenye fainali ya Carabao Cup...

Messi afunga mawili dhidi ya Bilbao na kubeba Barcelona...