Michezo

MIAMBA: Ureno yakanyaga Uholanzi na kutwaa taji la Uefa Nations League

June 11th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

PORTO, URENO

URENO walijinyakulia taji la pili la haiba kubwa chini ya kipindi cha miaka mitatu baada ya kuwapepeta Uholanzi 1-0 katika fainali ya Nations League mnamo Jumapili.

Chini ya kocha Fernando Santos, Ureno walitia kapuni taji la Euro 2016 baada ya kuwazidi ujanja Ufaransa waliokuwa wenyeji wa kipute hicho.

Bao la pekee na la ushindi kwa upande wa Ureno katika mchuano huo uliotandazwa mjini Porto lilifumwa wavuni na mchezaji Goncalo Guedes kunako dakika ya 60.

“Kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, kikosi kizima cha Ureno kimekuwa kikicheza kama familia. Ushindi huu wa Nations League ni ithibati kwamba umoja ni nguvu. Ushirikiano umetuwezesha kuudhihirishia ulimwengu mzima kuhusu ukubwa wa uwezo tulionao,” akasema Santos.

Bao la Guedes lilikuwa zao la ushirikiano kati yake na kiungo matata wa Manchester City, Bernardo Silva ambaye pia alimfanyiza kipa Jasper Cillessen wa Uholanzi kazi nyingi za ziada katika kipindi cha pili.

Ingawa Uholanzi walipania kurejea mchezoni katika dakika ya 65, jitihada za fowadi Memphis Depay ziliambulia pakavu baada ya kuzidiwa maarifa na kipa nambari moja wa Wolves, Rui Patricio ambaye alimnyima kiungo wa zamani wa Middlesbrough Marten de Roon nafasi nyingi za wazi.

Uingereza walikamilisha kampeni za Nations League katika nafasi ya tatu baada ya kuwachabanga Uswisi 6-5 mjini Guimaraes. Mshindi wa mchuano huo aliamuliwa kupitia mikwaju ya penalti baada ya pande zote mbili kuambulia sare tasa kufikia mwisho wa muda wa kawaida.

Kabla ya kipenga cha kuashiria mwanzo wa mechi hiyo kupulizwa, macho yote yalielekezwa kwa fowadi Cristiano Ronaldo wa Ureno na beki Virgil van Dijk wa Uholanzi.

Wawili hawa walikuwa tegemeo kubwa kambini mwa klabu zao katika kampeni za msimu huu. Ronaldo aliwaongoza Juventus kutia kibindoni ufalme wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A). Kwa upande wake, Van Dijk ambaye ni beki ghali zaidi duniani kwa sasa, alichangia pakubwa ufanisi wa Liverpool walionyanyua Kombe la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa mara ya sita na kukomesha ukame wa miaka saba bila taji lolote kabatini mwao.

 

 

Goncalo Guedes (kushoto) awania mpira dhidi ya kiungo Frenkie De Jong, katika fainali ya Uefa Nations League iliyokutanisha wenyeji Ureno na Uholanzi Juni 9, 2019, uwanjani Dragao, Porto. Picha/ AFP

Ronaldo, 34, aliyefunga jumla ya mabao matatu kwenye nusu-fainali iliyowakutanisha na Uswisi, alipoteza nafasi mbili za wazi dhidi ya Uholanzi japo kwa mara kadhaa, alidhibitiwa vilivyo na Van Dijk.

Fowadi huyo wa zamani wa Real Madrid anajivunia kuwafungia Ureno jumla ya mabao 88 hadi kufikia sasa katika soka ya kimataifa.

Ureno kwa sasa wanajivunia rekodi ya kutoshindwa katika jumla ya michuano 10 iliyopita. Uholanzi ambao walishindwa kufuzu kwa fainali za Euro 2016 na Kombe la Dunia mnamo 2018, angalau walipata jambo la kuwaliwaza tangu kocha Ronald Koeman apokezwe mikoba ya kikosi hicho.

Fainali ya Nations League msimu huu zinatarajiwa kutoa jukwaa mwafaka zaidi kwa makocha wa klabu mbalimbali za bara Ulaya kutambua baadhi ya wachezaji watakaopania kusajili kwa minajili ya kampeni za msimu ujao.

Kiungo matata wa Ureno, Bruno Fernandes, 24, anahusishwa pakubwa na uwezekano wa kujiunga na Manchester United au Tottenham Hotspur ambao wako radhi kutoa kima cha Sh9.5 bilioni. Nyota huyo aliwafungia Sporting Lisbon jumla ya mabao 32 na kuchangia 17 mengine katika kampeni za msimu uliopita.

Beki wa Uholanzi Matthijs de Ligt, 19, ni mchezaji mwingine ambaye anawaniwa pakubwa, huku akihusishwa na uwezekano wa kutua Man-United, Barcelona au Liverpool. Chipukizi huyo ambaye ni nahodha wa Ajax, aliwaongoza waajiri wake kunyanyua mataji mawili msimu huu.