Habari

Miamba wa KCPE 2015 wakosa kuwika KCSE 2019

December 18th, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

WANAFUNZI waliokuwa bora kwenye mtihani wa darasa la nane (KCPE) miaka minne iliyopita hawakutajwa miongoni mwa kumi bora kwenye mtihani wa kidato cha nne (KCSE) matokeo yalipotolewa Jumatano.

Mwanafunzi bora kwenye KCPE mwaka wa 2015 alikuwa Wabuko Aggrey Akhanyinya (pichani juu), aliyepata alama 449 na akajiunga na shule ya wavulana ya Alliance. Kwenye matokeo hayo, Wabukho Tony wa shule ya wavulana ya Kapsabet alitajwa kuwa bora nchini.

Msichana bora kwenye KCPE 2015, Felistus Onduso aliyepata alama 445 na kujiunga na shule ya wasichana ya Alliance pia hakutajwa kwenye orodha ya wanafunzi bora kwenye matokeo ya KCSE mwaka huu.

Wengine ambao waliokuwa kwenye orodha ya wanafunzi bora katika KCPE ya 2015 ni Macharia Wilson Muraga, Ruaraka aliyekuwa na alama 446, Nderi Nelly Muthoni (443), Naomi Gakui (442), Faith Joy (442), Janice Mutinda (441), Finley Ogechi (441) na Magret Amwayi (441).

Huku waliowika kwenye KCPE 2015 wakikosa kuongoza kwenye KCSE, waliopata chini ya alama 200 na kujiunga na shule za mashinani walitia fora.

“Uchanganuzi wetu wa jinsi watahiniwa waliopata alama za chini kama 177 walivyoweza kupata alama za juu katika KCSE ni masimulizi ya matumaini makuu na kutia moyo hasa katika wakati huu wa sera ya serikali inayoruhusu watahiniwa wote wa KCPE kujiunga na kidato cha kwanza,” akasema Bw Magoha.

Baadhi yao waliopata matokeo mabaya katika KCPE lakini wakawika KCSE ni pamoja na Kinyua Milka Wanjiru kutoka shule ya upili ya Gathara aliyepata alama 179 kwenye KCPE na kuzoa B- kwenye KCSE, Munyoki Mwikali aliyekuwa na alama 199 katika KCPE lakini akapata alama ya B- kwenye KCSE japo alisomea shule ya kibinafsi ya Mama Malia.

Wengine ni Sharon Cheopkoech aliyepata alama 183 kwenye KCPE na akapata alama ya C+ akisomea shule ya upili ya Saire, Mbugua R Macharia aliyesomea ya upili ya Kiambaa alipata alama C+ kwenye KSCE japo alipata alama 169 kwenye KCPE.

Bw Magoha alisema hii ni funzo kwa wazazi kwamba hawafai kuwakemea watoto wao wanapopata alama za chini kwenye mtihani.

“Wazazi wanafaa kuwasherehekea na kuwahimiza watoto wao kwa kila alama wanayopata,” alisema.