Michezo

'Miamba wa soka' wanyanyua kombe la EPL baada ya miaka 30

July 24th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MABINGWA Liverpool walisherehekea kupokezwa kombe la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30 mwishoni mwa mechi iliyowashuhudia wakiwafunga Chelsea jumla ya mabao 5-3 uwanjani Anfield.

Nahodha Jordan Henderson ambaye kwa sasa anauguza jeraha la paja, alipokezwa taji la Liverpool kutoka kwa mkufunzi wao wa zamani Sir Kenny Dalglish katika eneo mahsusi lililojengwa uwanjani Anfield kwa minajili ya shughuli hiyo.

Ushindi wa Liverpool dhidi ya Chelsea uliendeleza rekodi ya kutoshindwa kwa masogora wa kocha Jurgen Klopp katika uwanja wao wa nyumbani katika jumla ya misimu mitatu iliyopita kwenye soka ya EPL.

Chelsea kwa sasa wanahitaji alama moja pekee kutokana na mchuano wao wa mwisho wa msimu huu dhidi ya Wolves ili kujipa uhakika wa kukamilisha kampeni za msimu huu ndani ya mduara wa nne-bora na hivyo kufuzu kwa kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao.

Ikiwa Chelsea watazidiwa maarifa na Wolves, nao Leicester City wawaangushe Manchester United katika mchuano wao wa mwisho uwanjani King Power, basi Chelsea wataambulia nje ya mduara wa nne-bora msimu huu. Hata hivyo, bado watapata fursa ya kunogesha kivumbi cha UEFA iwapo wataibuka mabingwa wapya wa Kombe la FA katika fainali itakayowakutanisha na Arsenal uwanjani Wembley, Uingereza mnamo Agosti 1, 2020.

Chini ya kocha Frank Lampard, Chelsea kwa sasa wanashikilia nafasi ya nne kwa alama 63 sawa na Manchester United walioambulia sare ya 1-1 dhidi ya West Ham United uwanjani Old Trafford. Leicester wanakamata nafasi ya tano kwa alama 62. Watatu hao wanapigania nafasi mbili zilizoachwa na Liverpool na Manchester City katika vita vya kufuzu kwa gozi la UEFA msimu ujao wa 2020-21.

Liverpool walifungua ukurasa wao wa mabao kupitia kwa Naby Keita kunako dakika ya 23 kabla ya beki Trent Alexander-Arnold kupachika wavuni goli la pili katika dakika ya 38. Georginio Wijnaldum aliyafanya mambo kuwa 3-0 kabla ya mvamizi wa zamani wa Arsenal, Olivier Giroud kuwarejesha Chelsea mchezoni mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Hata hivyo, matumaini yao hayo yalizamishwa na Roberto Firmino aliyewafungia Liverpool bao la nne katika dakika ya 54 baada ya kushirikiana vilivyo na Alexander-Arnold.

Ujio wa chipukizi Christian Pulisic katika kipindi cha pili ulichangia ufufuo wa makali ya Chelsea waliofunga mabao mawili ya haraka kupitia kwa Tammy Abraham na Pulisic aliyefanya mambo kuwa 4-3 kufikia dakika ya 73.

Fataki zilizokuwa zikifyatuliwa na mashabiki waliokuwa wameanza kukongamana nje ya uwanja wa Anfield zilionekana kuwatia hamasa vijana wa Liverpool waliofunga bao la tano kupitia kwa Alex Oxlade-Chamberlain aliyekamilisha krosi ya Andy Robertson kwa ustadi mkubwa katika dakika ya 84.

Licha ya uwanja kuwa mtupu bila mashabiki, Liverpool walisherehekea ubingwa wao wa kwanza wa EPL ambao walikuwa wamesubiri kwa miaka 30.

Mohamed Salah angalifunga mabao matatu katika mechi hiyo na kuweka hai matumaini ya kutawazwa taji la mfungaji bora msimu huu. Hata hivyo, alipoteza nafasi nyingi za wazi alizoandaliwa na Keita katika kipindi cha kwanza kilichotamalakiwa na Chelsea.

Bao la Firmino lilichangiwa na Alexander-Arnold aliyevunja rekodi yake mwenyewe kwa kuchangia mabao 13 msimu huu, hii ikiwa idadi kubwa zaidi kuwahi kuchangiwa na beki katika msimu mmoja wa EPL.

Liverpool kwa sasa wamejizolea alama 55 kutokana na jumla ya 57 ambazo walikuwa na uwezo wa kujinyakulia uwanjani Anfield msimu huu baada ya kusajili ushindi mara 18 na kuambulia sare moja katika mechi 19 za ligi walizozichezea katika uwanja wao wa nyumbani.

Liverpool kwa sasa wanajiandaa kufunga rasmi kampeni za EPL msimu huu dhidi ya Newcastle United mnamo Julai 26 uwanjani St James Park.