Mibabe kutoana kijasho leo

Mibabe kutoana kijasho leo

MANCHESTER, Uingereza

Na MASHIRIKA

Mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza, zitapamba moto leo wakati miamba Manchester City, Liverpool na Chelsea watakuwa wenyeji wa Wolves, Aston Villa na Leeds mtawalia.

Mabingwa watetezi na viongozi City wanafukuzia ushindi wa sita mfululizo ligini msimu huu. Vijana wa Pep Guardiola wana asilimia kubwa ya kutamba ugani Etihad, hasa baada ya kuumiza Wolves msimu uliopita. Hata hivyo, City walipoteza 2-1 dhidi ya Leipzig kwenye Klabu Bingwa Ulaya Jumanne.

Kilikuwa kichapo cha kwanza cha City baada ya kuzoa ushindi mara saba mfululizo katika mashindano yote.Nambari nane Wolves wameokota alama mbili kutoka michuano mitatu iliyopita ya ligi. Bernardo Silva na Raul Jimenez watategemewa na City na Wolves mtawalia.

City itapoteza uongozi ikitoka sare ama kuchapwa nayo Liverpool iking’ute Villa uwanjani Anfield. Vijana wa Jurgen Klopp watawinda ushindi wa saba mfululizo katika mashindano yote na wa tatu dhidi ya Villa. Washambuliaji Mohamed Salah na Ollie Watkins wana mzigo mkubwa wa kutafutia Liverpool na Villa ushindi mtawalia.

Chelsea ilizidiwa ujanja na West Ham 3-2 ligini na kukabwa 3-3 dhidi ya Zenit kwenye Klabu Bingwa Ulaya katika mechi mbili zilizopita. Vijana wa Thomas Tuchel watatumai kujinyanyua dhidi ya nambari 15 Leeds ambayo imepoteza ugani Stamford Bridge mara nne mfululizo.

Macho yatakuwa kwa wachana-nyavu matata Mason Mount na Daniel James mtawalia. City, Liverpool na Chelsea zimezoa alama 35, 34 na 33 mtawalia. Ugani Emirates, nambari saba Arsenal itaalika Southampton makini kufuta vipigo dhidi ya Manchester United na Everton katika mechi ilizotupa uongozi.

Vijana wa Mikel Arteta wametoka sare dhidi ya nambari 16 Southampton mara mbili mfululizo kwa hivyo si mchuano rahisi. Nambari sita Manchester United inazuru wavuta-mkia Norwich ikatumai kuwazamisha kwa mara ya tano mfululizo.

You can share this post!

Leicester inafaa kujilaumu kubanduliwa Ligi ya Uropa

DOUGLAS MUTUA: Sudan hatarini kutekwa na jeshi kama Misri

T L