Michezo

Michezo Kenya kuanza upya corona ikithibitiwa

June 18th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

WAZIRI wa Michezo, Balozi Amina Mohamed amesema muda wa marufuku dhidi ya mikusanyiko ya hadhara uliotolewa na Rais Uhuru Kenyatta, utatumika kuweka mikakati zaidi ya jinsi ya kurejelea michezo wakati huu wa janga la corona.

Licha ya kutaathiri zaidi sekta ya michezo, Rais aliongeza kipindi cha marufuku ya mikutano ya umma kwa mwezi mmoja zaidi mnamo Juni 6, 2020 katika juhudi za kudhibiti maambukizi zaidi ya virusi vya homa ya corona.

“Tumeunda kamati ambayo itafanya kazi kwa muda wa wiki tatu zijazo. Wanakamati watatushauri kuhusu taratibu tunazostahili kuzitekeleza viwanjani ili tuanze upya kushiriki michezo mbalimbali,” akatanguliza Amina.

“Ilivyo, sioni uwezekano wa kurejelewa kwa shughuli zozote za michezo kabla ya muda wa siku 30 zilizoongezwa na Rais Uhuru Kenyatta kukamilika,” akaongeza.

Kamati iliyoundwa mnamo Juni 8, itatwikwa jukumu la kuzuru kaunti mbalimbali za humu nchini kushauriana na washikadau ili kukusanya maoni yatakayoelekeza Wizara katika kuamua muda mwafaka zaidi wa kuanzisha michezo tena humu nchini.

Katika hotuba yake kwa taifa mnamo Juni 6, 2020, Rais Uhuru Kenyatta alisisitiza kwamba maamuzi hayo ya kutolegeza kabisa baadhi ya kanuni za kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 yalikuwa zao la mashauriano ya kina na wataalamu wa afya.

Wizara ya Afya inatarajiwa sasa kushirikiana vilivyo na ile ya Michezo ili kubuni na kutathmini mipangilio ya itakayowezesha michezo mbalimbali kurejelewa kwa chini ya uzingativu wa kanuni na sheria zilizowekwa.